Jihadul Islami: Wazayuni wametangaza vita kwa kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina ya Jihadul Islami imetangaza kuwa, hatua ya Wazayuni ya kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu ni kutangaza vita dhidi umma wa Kiislamu.
Hayo yameelezwa na Ahmad al-Muudallal, mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina na kusisitiza kwamba, uvamizi wa walowezi wa Kizayuni na hatua yao ya kishenzi ya kuchoma moto nakala za kitabu kitukufu ya Qur'ani ni jinai na ni kuhujumu itikadi zetu na wakati huo huo ni kutangaza vita dhidi ya umma wa Kiislamu na Kiarabu.
Amesisitiza kuwa, muuqawama wa Palestina hausamima na kuweka mikono nyuma mkabala wa vitendo kama hivi vya Wazayuni bali utatoa majibu mwafaka.
Walowezi wa Kizayuni wenye misimamo mikali ya kufurutu ada wamevamia msikiti mmoja na kuvunjia heshima Qurani Tukufu katika mji wa Nablus, eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Kanda ya kamera ya CCTV imeonyesha namna walowezi hao wa Kizayuni wenye misimamo mikali walivyoshambulia eneo hilo takatifu la Waislamu katika kijiji cha Urif, yapata kilomita 13 kusini mwa Nablus.
Video hiyo imewaonyesha Wazayuni hao waliokuwa wamefunika nyuso zao wakichana na kuchoma moto nakala za Qurani Tukufu ndani ya msikiti huo. Walowezi hao wa Kizayuni hawakuishia hapo, walienda mbali zaidi na kuingiza mbwa ndani ya msikiti huo.