Taliban:Tungekubali kuwa watumwa wa Marekani serikali yetu ingekuwa imeshatambuliwa
Msemaji wa serikali ya Taliban amejibu shutuma za baadhi ya maafisa wa serikali ya zamani ya Afghanistan kuhusiana na uhusiano wa nchi hiyo na Marekani na kusema: "kama tungekuwa tunaendeshwa na Marekani, tungekuwa tayari tumeshatambuliwa".
Zabihullah Mujahid amejibu lawama zilizotolewa kuhusiana na uhusiano wa Afghanistan na Marekani kwa kusisitiza kwamba, Taliban iko huru katika maamuzi yake inayochukua na hiyo ina maana ya uhuru badala ya utumwa na kuongeza kuwa, kama Taliban ingekubali kuwa mtumwa, ingekuwa imeshatambuliwa.
Zabihullah Mujahid amewahutubu viongozi wa serikali ya zamani ya Afghanistan kwa kusema: "hapo kabla, maelfu ya wanajeshi wa Marekani walikuwa wakiranda ndani ya nchi yenu na nyinyi mkawa mnapokea dola mkabala wa kukufanyeni watumwa wao. Mkabala wa hilo na kwa muda wote wa miaka 20 mlikuwa mkipeleleza nyumba za ndugu zenu Waislamu, mkivamia nyumba zao na kuwapiga mabomu pamoja na kuwafanyia dhulma, lakini leo hii nchi yenu inajitegemea katika uchukuaji wa maamuzi yake yote, na hii ndio maana ya uhuru; si kufanywa watumwa".
Msemaji wa serikali ya Taliban ameendelea kueleza kwamba, laiti kama Taliban ingekuwa na mfungamano na Marekani, isingewekewa vikwazo vya kidhalimu.
Itakumbukwa kuwa kundi la Taliban liliingia madarakani nchini Afghanistan Agosti 15, 2021 baada ya kuiondoa madarakani serikali ya Mohammad Ashraf Ghani.
Kwa sasa, Afghanistan inakabiliwa na hali mbaya ya kiuchumi na kibinadamu iliyosababishwa na athari za kukaliwa kwa mabavu kwa muda wa miaka 20 na jeshi la Marekani na vita vilivyotokana na uvamizi huo. Uvamizi, vita na kukaliwa kijeshi vimeharibu na kuangamiza miundombinu ya kiuchumi ya Afghanistan.
Katika hali hiyo, baada ya Marekani kuondoka kimadhila nchini Afghanistan mwishoni mwa Agosti 2021 kulikofuatiwa na Taliban kuingia madarakani, Washington imetumia kisingizio hewa na cha uwongo kuzuia na kuhodhi karibu dola bilioni 10 mali na milki za watu wa Afghanistan na kuiwekea vikwazo nchi hiyo vilivyopelekea hali ya raia wake kuwa mbaya zaidi.
Wakati huo huo, matakwa na masharti muhimu zaidi ya kimataifa kwa Taliban ili kuitambua serikali ya kundi hilo ni kuundwa serikali jumuishi, kuheshimiwa haki za raia ikiwa ni pamoja na kutambua haki ya wanawake ya kufanya kazi na ya kupata elimu wasichana wa Afghanistan.../