Ongezeko lisilokuwa la kawaida la idadi ya kampuni zilizofilisika laripotiwa Ulaya
(last modified Fri, 18 Aug 2023 08:17:30 GMT )
Aug 18, 2023 08:17 UTC
  • Ongezeko lisilokuwa la kawaida la idadi ya kampuni zilizofilisika laripotiwa Ulaya

Idadi ya makampuni yaliyofilisika barani Ulaya imefikia kiwango cha juu zaidi tangu 2015.

Kituo cha Takwimu cha Umoja wa Ulaya (Eurostat) kilitangaza jana Alhamisi kwamba kwa mara ya sita mfululizo, idadi ya makampuni yaliyofilisika katika umoja huo imeongezeka, na kwamba suala hilo linatambuliwa kuwa rekodi nyingine tangu 2015.

Eurostat imesema kwamba, idadi ya makampuni ya Ulaya yaliyofilisika imeongezeka kwa 8.4% katika robo ya pili ya 2023 ikilinganishwa na robo ya kwanza ya mwaka huu.

Taarifa ya Kituo cha Takwimu cha Umoja wa Ulaya inasema, sekta za malazi na huduma za chakula ambazo zimesajili asilimia 23.9 ya taarifa za kufilisika, sekta za usafirishaji na uhifadhi asilimia 15.23, na sekta za elimu na shughuli za kijamii zenye asilimia 10.1, mtawalia, ndizo zilizoathiriwa zaidi.

Eurostat pia imetangaza kwamba, idadi ya matangazo ya kufilisika katika Jumuiya ya Ulaya katika robo ya pili ya 2023 yalikuwa mengi zaidi kuliko robo ya mwisho ya 2019, kabla ya janga la Covid-19, na ongezeko kubwa la kufilisika kati ya vipindi hivi viwili linaweza kuonekana katika sekta ya malazi kwa asilimia 82.5.

Nchi za Ulaya zinasumbuliwa sana na matatizo ya kiuchumi hasa kutokana na vita vinavyoendela kati ya Russia na Ukraine na kutengwa misaada mikubwa ya silaha na fedha ya nchi hizo kwa serikali ya Kiev dhidi ya Moscow.