Mkuu wa Wagner aaga dunia katika ajali ya ndege nchini Russia
Kiongozi wa kundi la wanamgambo wa Wagner, Yevgeny Prigozhin ameripotiwa kuaga dunia katika ajali ya ndege huko kaskazini magharibi ya Russia.
Press TV imenukuu kanali ya habari ya Russia Today ikiripoti habari hiyo na kueleza kuwa, Prigozhin aliaga dunia baada ya ndege ya kibinafsi iliyokuwa ikitoka Moscow kuelekea St Petersburg kuanguka karibu na kijiji cha Kuzhenkino katika eneo la Tver, kaskazini magharibi ya Russia.
Aidha shirika rasmi la habari la Russia RIA Novosti limenukuu mamlaka za safari za ndege nchini humo zikisema kuwa, Prigozhin na watu wengine tisa waliokuwa kwenye ndege hiyo wamepoteza maisha.
Kanali ya Grey Zone yenye mfungamano la Kundi la Wagner imeripoti kuwa: Mkuu wa Kundi la Wagner, Shujaa wa Russia, mzalendo halisi, Yevgeny Viktorovich Prigozhin ameaga dunia kutokana na vitendo vya wasaliti wa Russia.
Aidha Wizara ya Hali za Dharura ya Russia imesema watu wote kumi akiwemo Prigozhin wameaga dunia kwenye ajali hiyo iliyohusisha ndege binafsi aina ya Embraer Legacy.
Ikumbukwe kuwa, vikosi vya Wagner vilihamishiwa Belarus mwezi Juni mwaka huu baada ya uasi uliozuka dhidi ya serikali ya Russia.
Kundi hilo la wanamgambo wa Wagner ambao walihusika pakubwa vitani huko Ukraine walifanya uasi na kudhibiti mji wa Rostov-on Don na kuanza kuelekea katika mji mkuu Moscow, kabla ya kufikiwa makubaliano yaliyohitimisha uasi wao.