Siku ya Kimataifa ya Quds: Palestina, Kadhia Kuu ya Waislamu Duniani
Mbunge wa ngazi za juu nchini Iran amesema kadhia ya Palestina ndio muhimu zaidi kwa Waislamu na hivyo ametoa wito wa ushiriki mkubwa katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds.
Sayyid Hossein Naqavi ambaye pia ni msemaji wa Tume ya Sera za Kigeni na Usalama wa Taifa katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, amesema kujitokeza kwa wingi watu katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds, kutatuma ujumbe kwa mara nyingine kuwa, kadhi ya Palestina ndio kadhia muhimu zaidi kwa Waislamu duniani.
Ameongeza kuwa, madola yenye kiburi duniani hasa Marekani na Utawala wa Kizayuni wa Israel pamoja na kibaraka wao, Saudi Arabia, yamekuwa yakifanya njama za kutenga kadhia ya Palestina miongoni mwa Waislamu kwa kizusha hitilafu za kimadhehebu na machafuko katika nchi za Kiislamu kupitia makundi ya magaidi wakufurishaji.
Naqavi Hosseini amesema kutokana na njama hizo, kadhia ya Palestina haizingatiwa ipasavyo katika ulimwengu wa Kiislamu hasa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Hata hivyo amesisitiza kuwa, Waislamu kote duniani kwa kushiriki kwa wingi katika maandamano na mijumuiko ya Siku ya Kimataifa ya Quds, wataifanya dunia iangazie jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel na kuifanya kadhia ya Palestina kuwa kipaumbele cha kwanza katika ulimwengu wa Kiislamu.
Ijumaa ya mwisho la kila mwezi mtukufu wa Ramadhani huadhimishwa kama Siku ya Kimataifa ya Quds kufuatia pendekezo la Imam Khomeini MA, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika siku hiyo Waislamu na watetezi wote wa haki kote duniani hujumuika pamoja katika maandamano na mikutano ambayo huangazia kadhia ya ukombozi wa Palestina sambamba na kulaani jinai za utawala ghasibu wa Israel. Mwaka huu Siku ya Kimataifa ya Quds itaadhimishwa tarehe Mosi Julai.