Kukiri kwa Borrell kwamba nchi zinazoendelea zinatafuta mbadala wa Magharibi
Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, ameandika katika makala iliyochapishwa kwenye blogu yake akisema: "Sheria zinazotawala dunia zinachakaa na nchi zinazoendelea za kusini mwa dunia zinatafuta mbadala wa Magharibi."
Borrell amekiri kwamba: Hii leo katika Amerika ya Kusini, Afrika, Mashariki ya Kati, Afrika Kaskazini, na bila shaka katika Asia, karibu wote wanafikiri kwamba, kuna mbadala wa kutegemewa ghairi ya Magharibi, si tu kiuchumi, lakini pia kiufundi, kijeshi, na kiitikadi.
Kukiri kwa Borrell juu ya kuwepo juhudi za nchi zinazoendelea za kutafuta mbadala wa madola ya Magharibi kunakuwa na maana zaidi kwa kuzingatia mwelekeo jumla wa sasa wa ulimwengu, ambao unaelekea kwenye dunia ya kambi kadhaa, na wakati huo huo kupunguza udhibiti na ushawishi wa nchi za Magharibi.
Kuhusu mabadiliko yanayotokea barani Afrika na juhudi za nchi zinazoendelea za kutafuta "washirika wapya badala ya mtindo wa Magharibi", Mkuu huyo wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya amedai kuwa: "Wachezaji hawa wapya (badala ya mtindo wa Magharibi) hawawaulizi watawala wa nchi hizo kwamba ni watu gani walioko magereza au utajiri wa nchi hizo unakwenda wapi, na suala hili linawafurahisha wengi wa watawala hawa." Kwa njia hii, Borrell amejaribu kuhusisha mwelekeo wa sasa wa nchi zinazoendelea wa kuyapa mgongo madola ya Magharibi, ikiwa ni pamoja na Afrika, na kutojali kwa mataifa washindani wa Magharibi kama vile Uchina na Russia kuhusu masuala ya haki za binadamu na ufisadi wa kifedha. Hii ni licha ya kwamba, katika baadhi ya nchi zinazoendelea waitifaki wa Marekani na Magharibi kwa ujumla, kunashuhudiwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, na ufisadi wa kifedha hutokea mara kwa mara katika nchi hizo bila kukabiliwa na jibu athirifu kutoka kwa nchi za Magharibi.
Suala la nchi zinazoendelea kuiacha mkono Magharibi na kutafuta njia mbadala pia limeibuliwa na viongozi wa juu wa nchi za Magharibi kama Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron. Katika hotuba yake kwenye Mkutano wa Usalama wa Munich Februari 2020, Emmanuel Macron alikiri kwamba, nafasi ya Magharibi katika uga wa kimataifa imedhoofika na mizani ya nguvu duniani imebadilika kutokana na kuibuka kwa madola mapya yenye nguvu. Macron alisema: "Tunaweza kuona udhaifu fulani wa Magharibi. Maadili yamebadilika na nguvu mpya zimeibuka."
Hivi sasa, kuna mpambano kati ya madola yanayodhibiti masuala mengi ya dunia ya Magharibi na madola washindani wao katika ngazi ya kimataifa. Kwa karne kadhaa, Wamagharibi wametawala dunia na daima wamekuwa wakiwanyonya watu na mataifa mengine, wakati wa ukoloni na katika zama za ubeberu wao. Wakati wa Vita Baridi na baada yake, Marekani ikiwa kiongozi wa nchi za Magharibi, ilifanya juhudi kubwa kupanua udhibiti wake ulimwenguni. Hata hivyo, hali ya ulimwengu na mfumo wa kimataifa umepitia mabadiliko ya kimsingi, na sasa viongozi wa nchi za Magharibi wanakiri wenyewe kwamba, kipindi cha udhubiti wa Magharibi kimepita na kuyoyoma. Katika kipindi cha baada ya Vita Baridi, mwelekeo wa kimataifa katika nyanja mbalimbali umepelekea kuibuka nguvu kubwa za kiuchumi, kisiasa na kijeshi kama vile Russia, Uchina, na India katika nyanja ya kimataifa, licha ya jitihada kubwa zilizofanywa na Marekani na washirika wake kwa ajili ya kudumisha ushawishi wao na mfumo wa kambi moja duniani. Nguvu hizo mpya zinazoibuka katika mfumo wa taasisi kama vile BRICS, Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai au Jumuiya ya Kiuchumi ya Eurasia, zinafanya jitihada za kuanzisha mwelekeo mpya katika siasa za ulimwengu, uchumi, biashara na fedha.
Kwa sasa Magharibi, ikiongozwa na Marekani, inakabiliwa na washindani kama China na Russia. China ambayo sasa ni nchi ya pili yenye nguvu kubwa zaidi za kiuchumi duniani baada ya Marekani, inatarajiwa kuwa nguvu kubwa zaidi ya kiuchumi duniani na kuitimulia kivumbi Marekani ifikapo mwaka 2030, na suala hili linaibua alama kubwa ya kuuliza kuhusu uongozi wa kiuchumi na kibiashara wa nchi za Magharibi hususan Marekani. Russia pia, baada ya kipindi cha kuzorota katika miaka ya 1990, tangu mwaka 2000 na baada ya Vladimir Putin kuchukua madaraka, ilianzisha mchakato wa kujisasisha na kujijenga upya, na sasa ni mpinzani mkuu wa kisiasa na kijeshi wa Magharibi, hasa Marekani.
Nukta muhimu zaidi ni kwamba, kuporomoka nguvu na ushawishi wa nchi za Magharibi katika upeo wa kimataifa kunatokana kwa kiasi kikubwa na mienendo na utendaji usio sahihi wa Wamagharibi duniani kote ambao wameyakandamiza mataifa yaliyokuwa chini ya utawala wao katika karne za hivi karibuni kupitia sera zao za kikoloni na kibeberu. Suala hili linaonekana zaidi kuhusiana na nchi zinazoendelea, ambazo nyingi zimekuwa chini ya utawala na ukoloni wa madola ya Magharibi kwa muda mrefu sana. Agosti mwaka 2019 Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ilisema katika muktadha huu kwamba: Hivi sasa tunaishi kwenye ukingo wa kumalizika kipindi cha udhibiti wa Magharibi duniani, na suala hili limesababishwa na makosa ya huko nyuma ya Magharibi.
Naam, nchi zilizochoshwa na mifumo, sera, siasa na mienendo ya kindumakuwili na kinafiki ya Magharibi, sasa zinatafuta njia mbadala ya kutegemewa, na hili ni tatizo ambalo hata Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, amelazimika kuafikiana nalo.