Ripoti ya Congress ya Marekani Kuhusu Tukio la Benghazi, Libya
https://parstoday.ir/sw/news/world-i10270-ripoti_ya_congress_ya_marekani_kuhusu_tukio_la_benghazi_libya
Baada ya kukamilika mchakato wa vyama viwili vikuu vya Marekani vya Democrat na Republican kuwateua wagombe wao ambao watawania kiti cha urais yaani Hilary Clinton na Donald Trump kwa utaratibu, pande mbili sasa zimeanza kuchafuana katika kampeni.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 30, 2016 07:20 UTC
  • Ripoti ya Congress ya Marekani Kuhusu Tukio la Benghazi, Libya

Baada ya kukamilika mchakato wa vyama viwili vikuu vya Marekani vya Democrat na Republican kuwateua wagombe wao ambao watawania kiti cha urais yaani Hilary Clinton na Donald Trump kwa utaratibu, pande mbili sasa zimeanza kuchafuana katika kampeni.

Chama cha Republican kimekuwa cha kwanza kumchafulia jina mgombea wa Democrat Hilary Clinton.

Hivi karibuni Kamati ya Congress ya Marekani ilichapisha ripoti ya kurasa 800 kuhusu kuzembea utawala wa Rais Barack Obama katika kuwalinda wanadiplomasia wa nchi hiyo waliokuwa nchini Libya mwaka 2012 wakati ubalozi wa Marekani ulipovamiwa mjini Benghazi. Ubalozi huo pia ulikuwa ukitumiwa kama kituo cha Shirika Kuu la Kijasusi la Marekani CIA. Congress ilianzisha uchunguzi baada ya kusambazwa filamu ya namna wanamgambo walivyovamia ubalozi huo na kumuua balozi wa Marekani na wanadiplomasia wengine watatu. Congress inalaumu Jeshi la Marekani kwa kushindwa kuwapa ulinzi wa kutosha wanadiplomasia hao wanne.

Ripoti hiyo imesema kuwa, masaa manane baada ya ubalozi huo kushambuliwa, wanajeshi wa Marekani walikuwa bado hawajafika sehemu hiyo. Tukio hilo lilijiri wakati Hilary Clinton alipokuwa waziri wa mambo ya nje Marekani.

Ripoti hiyo ya Congress inasema wakati akiwa waziri wa mambo ya nje, Clinton aliandikiana barua na shirika la kijasusi la CIA kwa kutumia akaunti ya barua pepe au email yake binafsi badala ya kutumia ile aliyopewa na serikali. Ripoti hiyo imesema kwa kufanya hivyo, Clinton alihatarisha maisha ya raia wa Marekani.

Trey Gowdy, mbunge wa chama cha Republican aliyeongoza kamati hiyo ya uchunguzi kuhusu tukio la Benghazi amesema atafichua email hizo za Hillary Clinton na kuonyesha namna alivyozembea kikazi.

Kutangazwa ripoti hiyo ya kurasa 800 kumepelekea Ikulu ya White House kutoa tamko. Josh Earnest msemaji wa rais wa Marekani ameitaja ripoti hiyo kuwa yenye malengo ya kisiasa na isiyo sahihi.

Amesema wanachama wote wa kamati ya uchunguzi wamekiri kuwa Hilary Clinton hakuwa na hatia lakini wajumbe wa chama cha Republican wanataka kutumia kwa malengo ya kisiasa tukio hilo la kuuawa wanadiplomasia wanne.

Wademocrat na Warepublican wana mitazamo tafauti kuhusu ripoti hiyo ya tukio la Benghazi na kila mmoja anatumia ripoti hiyo kwa maslahi yake binafsi.

Uchunguzi wa maoni uliofanywa hivi karibuni umebaini kuwa Hilary Clinton na Donald Trump ni wagombea urais wanaochukiwa zaidi katika historia ya Marekani.

Kwa hivyo Wamarekani wataelekea katika masanduku ya kupigia kura mwezi Novemba wakiwa na wagombea hao wawili ambao wanachukiwa na umma nchini humo.

Hadi wakati wa uchaguzi wagombea hao wawili watatumia nukza dhaifu za upande wa pili kuchafuliana majina. Nukta dhaifu zaidi ya Hilary Clinton inahusiana na email alizotuma au kupokea kupitia akaunti yake binafsi ya email kuhusu tukio la Benghazi. Uchunguzi wa maoni unaonyesha kuwa, Clinton anawavutia wapiga kura wengi zaidi akilinganishwa na Trump na kwa msingi huo Warepublican wanatumia kadhia hiyo ya email kumchafulia jina.