Ujerumani yapinga usitishawaji vita huko Gaza
(last modified Sat, 14 Oct 2023 08:00:53 GMT )
Oct 14, 2023 08:00 UTC
  • Christian Wagner
    Christian Wagner

Ujerumani haikuunga mkono mpango wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF kwa ajili ya kusimamishwa vita huko Gaza.

Jumamosi iliyopita tarehe 7 Oktoba wapiganaji wa Muqawamawa Palestina walianzisha operesheni kubwa na ya kipekee inayoitwa Kimbunga cha al-Aqsa kutokea Gaza (kusini mwa Palestina) dhidi ya maeneo ya utawala wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA; Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani Christian Wagner Ijumaa ya jana hakuunga mkono mpango wa UNICEF wa kusitisha mapigano ili kuundaa njia salama ya kufikishwa misaada ya kibinadamu huko Gaza. Wagner amedai kuwa utawala wa Kizayuni una haki ya kujilinda.

Watoto wa Palestina mbele ya makao makuu ya UNICEF Ghaza 

Hii ni katika hali ambayo James Elder, Msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), amesema kuwa kunahitajika usitishwaji vita na eneo salama ili kulinda watoto  wa Ghaza.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani pia amekwepa kujibu swali kuhusu iwapo nchi hiyo imetaka kufanyike uchunguzi wa kimataifa kuhusu matumizi ya Isreal mabomu ya fosforasi dhidi ya wananchi wa Palestina.

Siku ya Alkhamisi, Kansela Olaf Schultz wa Ujerumani alikariri siasa za Berlin za kuunga mkono bila masharti utawala wa Kizayuni mbele ya wabunge wa nchi hiyo na kuongeza kuwa historia na uwajibikaji wa nchi hiyo kutokana na kile kinachodaiwa kuwa mauaji ya kimbari ya Holocaust unailazimu kutetea uwepo na usalama wa Israeli.

Utawala wa Kizayuni ambao juhudi zake za kusimamisha operesheni za muqawama huko Ghaza hazijafikia popote na wala hauna malengo maalumu kutokana na mashambulizi yake ya mabomu huko Ghaza, unaendelea kuwalenga kwa makusudi raia wa kawaida katika ukanda huo.

Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza katika ripoti yake ya karibuni kuhusu kuuawa shahidi raia 1,900 wakiwemo watoto 614 na wanawake 370 katika mashambulizi ya mabomu ya utawala huo wa Kizayuni.