Upinzani wa China kwa hatua ya Marekani ya kuishambulia kijeshi Yemen
Wang Wenbing, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesema, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halijatoa kibali kwa mtu yeyote kutumia nguvu dhidi ya Yemen, akimaanisha hujuma na mashambulio ya kijeshi yanayofanywa na Marekani na Uingereza dhidi ya ngome na vituo vya harakati ya Ansarullah ya Yemen.
Wenbing amesisitiza kuwa, mamlaka ya kujitawala na umoja wa ardhi za nchi za kandokando ya Bahari Nyekundu ikiwemo Yemen lazima viheshimiwe ipasavyo.
Msimamo huu wa China ni muhimu kwa sababu mara baada ya kupitishwa azimio hivi karibuni la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Yemen, Marekani na Uingereza zilianzisha mashambulizi dhidi ya nchi hiyo, ilhali azimio hilo halijatoa idhini kwa namna yoyote ile ya kutumiwa mabavu na nguvu za kijeshi dhidi ya Yemen.
Kwa hiyo, kwa mtazamo wa China, Marekani na Uingereza zinatumia fursa kwa manufaa yao na zinaishambulia Yemen kinyume na sheria za kimataifa; na hatua hiyo lazima ikomeshwe.
Kuhusiana na suala hili, mtaalamu wa masuala ya kimataifa na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Australia, Wen Ti Song, anasema: "Marekani, siku zote imekuwa ikilitumia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na maazimio yake kama wenzo tu.
Marekani inatumia kile inachodai kuwa ni maazimio ya Baraza la Usalama ili kuhalalisha mashambulizi yake. Ukweli ni kwamba, Washington imetoa tafsiri ya uwongo na ya upotoshaji kuhusu azimio la hivi karibuni la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Yemen".
Ukweli ni kwamba Marekani, Uingereza na waitifaki wao wengine zimeishambulia mara kadhaa Yemen kwa kisingizio cha kulinda usalama wa meli katika Bahari Nyekundu, na wakati huo huo zinatoa kauli za upayukaji za kuielekezea harakati ya Ansarullah ya Yemen tuhuma za kila aina, ilhali inachofanya harakati hiyo ya muqawama ya Yemen na kwa ajili ya kuwahami wananchi wa Gaza na muqawama wa Palestina dhidi ya mashambulizi ya utawala wa Kizayuni, ni kuzishambulia meli za Kizayuni pekee au zile zinazoelekea bandari za Palestina inayokaliwa kwa mabavu kwenye ardhi zilizopachikwa jina bandia la Israel.
Marekani, sio tu inazuia kusitishwa mapigano huko Gaza, lakini pia inatafuta fursa ya kulihodhi eneo pana la Bahari Nyekundu kupitia hatua yake ya kutuma manowari zake kwenye eneo hilo.
Kutokana na kubainika ukweli halisi kuhusu sababu ya kuwepo kijeshi Marekani katika eneo, ambayo ni kulinda uhai wa utawala bandia wa Kizayuni na kuidhibiti Bahari Nyekundu, hatua ambayo ni tishio kubwa kwa uhuru wa safari za baharini, jinai zinazofanywa na Marekani na Uingereza nchini Yemen zimekuwa zikishutumiwa na kulaaniwa kimataifa.
Kuhusiana na hili, Alfred Wu, Profesa Msaidizi katika Kitivo cha Sera za Umma cha Lee Kuan Yew katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Singapore, anasema: "Marekani yenyewe ni tishio kwa usalama wa dunia. Mahali popote walipopelekwa wanajeshi wa Marekani wamevuruga amani na usalama wa mahali hapo; na tunaweza kuashiria kuwepo kijeshi Marekani nchini Iraq na Syria na sasa hivi katika Bahari Nyekundu, ambapo lengo muhimu zaidi la Washington kuwepo huko ni kuudhibiti Mlango-Bahari wa Bab al-Mandab ili kulinda uhai wa Israel".
Alaa kulli haal, msimamo wa China, kwamba hakuna mtu aliyeipatia Marekani kibali cha kutumia nguvu dhidi Yemen una umuhimu kwa ajili ya kuzipa mwamko na uelewa fikra za walimwengu.
Hata hivyo, matarajio ya jamii ya kimataifa kwa China, kwa kuwa ni mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ni makubwa zaidi ya kuonyesha upinzani wa kidiplomasia tu.
China, ambayo inaagiza sehemu kubwa ya nishati inayohitajia kutoka Mashariki ya Kati na kusafirishwa kupitia Bahari Nyekundu, bila shaka yoyote inafahamu madhara ya kuvurugika usalama kwa kuwepo kijeshi Marekani katika eneo hilo muhimu la majini, na ikiwa ni mwanachama muhimu na wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ina jukumu na masuulia makubwa ya kukomesha uhalifu wa Marekani nchini Yemen. Kuhusiana na hilo, Beijing inao uwezo wa kutumia taasisi za kimataifa, ikiwa ni pamoja na Baraza la Usalama, kukomesha jinai hizo za Washington na washirika wake.../