Hatari za mitandao ya kijamii na juhudi za kuzitungia sheria
https://parstoday.ir/sw/news/world-i108010-hatari_za_mitandao_ya_kijamii_na_juhudi_za_kuzitungia_sheria
Katika miaka ya hivi karibuni, mitandao ya kijamii imekuwa sehemu isiyotenganishika na maisha ya mwandamu wa sasa, kwa kadiri kwamba, ni nadra sana kumpata mtu ambaye hajajiunga kwenye mitandao hiyo na kufuatilia masuala mbalimbali anayoyapenda na yanayoivutia nafsi yake.
(last modified 2026-04-26T10:08:53+00:00 )
Feb 05, 2024 00:18 UTC
  • Hatari za mitandao ya kijamii na juhudi za kuzitungia sheria

Katika miaka ya hivi karibuni, mitandao ya kijamii imekuwa sehemu isiyotenganishika na maisha ya mwandamu wa sasa, kwa kadiri kwamba, ni nadra sana kumpata mtu ambaye hajajiunga kwenye mitandao hiyo na kufuatilia masuala mbalimbali anayoyapenda na yanayoivutia nafsi yake.

Suala hili limegeuka kuwa sehemu ya maisha, hasa ya vijana chipukizi na mabarobaro. Wao hutumia muda wao mwingi  kufuatilia maudhui tofauti katika mitandao mbalimbali ya kijamii na kuhukumu juu ya masuala tofauti kulingana na taarifa wanazopata kuhusu masuala hayo katika mitandao hiyo.

Ulimwengu unatawaliwa na mitandao ya kijamii

Hii ni katika hali ambayo kiuhalisia, mitandao ya kijamii huwa ni fursa na vitisho kwa wakati mmoja kwa watumiaji wake katika nyanja mbalimbali. Lakini wasiwasi ambao hivi sasa umekuwa mkubwa zaidi ni athari mbaya na haribifu za mitandao ya kijamii katika nyanja za kisiasa, kijamii na kiuchumi kwa watu binafsi na jamii kwa ujumla.

Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni, idadi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii imepindukia watu bilioni tano, ambayo ni karibu 62% ya watu wote duniani.

Kulingana na ripoti iliyoandaliwa na mashirika ya ufuatiliaji wa vyombo vya habari ya Multiwater na wakala wa mitandao ya kijamii wa WeR Social, idadi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii iliongezeka kwa asilimia 5.6 mwaka wa 2023, ambayo ni zaidi ya asilimia 0.9 ya ongezeko la watu duniani. Ripoti hiyo inaonyesha kuwa, kati ya mitandao ya kijamii, Facebook imesajili idadi kubwa ya watumiaji, ukiwa ni moja ya mitandao tanzu ya Meta kwa kusajili watu bilioni mbili na milioni 190, na Instagram, ambayo pia inamilikiwa na Meta imeshika nafasi ya pili kwa kuwa na watumiaji bilioni moja na milioni 650. 

Ripoti zilizotolewa zinaonyesha kuwa watumiaji wa kila siku wa intaneti hutumia kwa wastani muda wa saa 6 na dakika 40 wakiwa katika intaneti, na asimilia 60 ya trafiki ya mtandao duniani imetumiwa na watumiaji wa simu za mkononi.

Upanuzi na uongezekaji huu wa mitandao ya kijamii ni  kengele kubwa ya hatari kwa jamii tofauti, hasa kwa watumiaji walio vijana chipukizi na mabarobaro. Kuongezeka  visa vya kujiua, msongo wa mawazo, hali za tafrani, ukatili wa kingono, utumiaji wa lugha chafu, ugomvi wa kuingiana maungoni, kupanuka ufa wa kitabaka na mizozo ya kikabila, ya mbari na ya kidini, ni miongoni mwa athari mbaya za matumizi ya mitandao ya kijamii ambazo zimezitia wasiwasi jamii mbalimbali duniani.

Akili iliyohodhiwa na jumbe mbalimbali

Kuongezeka kupita kiasi matumizi ya mitandao ya kijamii na kudhihirika wazi hatari na athari zake kwa mtu binafsi, jamii na uchumi kumezifanya nchi mbalimbali zifikirie kuchukua hatua za kuiwekea mipaka na kuidhibiti, bali hata kuitungia sheria mitandao hiyo na kupanga mbinu za kuibana bila kuhisika au hata kwa uwazi kabisa. 

Kuhusiana na jambo hilo, tunaweza kuashiria vikao vya Maseneta wa Marekani na wakuu wa mitandao mikubwa ya kijamii, wakiwemo wamiliki wa mashirika ya Meta, Snapchat, Discord, X na Tik Tok, ambavyo vilifanyika katika Seneti ya nchi hiyo. Katika vikao hivyo, Maseneta hao walikosoa dosari za kutodhaminiwa usalama wa vijana kimaadili kwenye mitandao hiyo ya kijamii.

Kwa kutoa mfano, Seneta wa Republican Lindsey Graham, aliashiria  shughuli za kampuni ya Meta na kumuelekea Mkurugenzi Mtendaji wake akimwambia: "Bwana Zuckerberg, wewe na mashirika yako mikono yenu imetapakaa damu, kwa sababu mna bidhaa zinazoua watu".

Ijapokuwa wakurugenzi wa mitandao ya kijamii daima wamekuwa wakitetea utendaji wao, lakini kubainika wazi athari mbaya za mitandao hiyo ni jambo ambalo haliwezi tena kufichika, kiasi kwamba katika kikao hicho, Mark Zuckerberg, Mkurugenzi Mtendaji wa Meta alionyesha majuto na kusikitishwa na yaliyotokea.

Bila shaka si Marekani pekee, bali hata barani Ulaya pia, viongozi wa serikali wamezungumzia mara kadhaa kuhusu uwekaji mipaka na kutunga sheria kali ili kudhibiti utumiaji wa mitandao ya kijamii hasa kwa vijana chipukizi, na kwenda mbali zaidi kwa kulitungia sheria suala hilo.

Ukweli ni kwamba, "kuiwekea utaratibu" mitandao ya kijamii na kutaka kuwepo uwazi katika shughuli za mtandao hiyo kwa ajili ya kuchunga usalama na maslahi ya taifa kunahesabiwa kuwa moja ya misingi muhimu na inayokubaliwa na nchi nyingi duniani. Nchi hizo, hivi sasa zimepitisha sera za kubana matumizi ya mitandao ya kijamii zinazojumuisha kuiwekea mashinikizo mitandao hiyo ya kuitaka iinue kiwango cha usalama kwa mtumiaji na kuwawekea mipaka ya utumiaji vijana wadogo na maborabaro. 

Gazeti la Politico la nchini Marekani limegusia utafiti uliofanywa kuhusu athari za mitandao ya kijamii kwa afya ya akili za watoto na vijana wadogo na kuandika kuwa: "nchi mbalimbali zimo mbioni kuuwekea mipaka na kuutungia sheria utumiaji wa majukwaa haya".

Kwa mujibu wa gazeti hilo, kuna mtazamo wa pamoja juu kuwepo uhusiano wa moja kwa moja kati ya matumizi ya mitandao ya kijamii na uzima wa akili ya vijana wadogo; na kwa sababu hiyo ndio maana nchi nyingi duniani zinajaribu kutumia mbinu tofauti ili kupunguza athari mbaya za mitandao ya kijamii kwa akili na fikra za watu wao hususan watoto na vijana wadogo.