UN: Iran ina nafasi chanya katika matukio ya Asia Magharibi
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameelezea wasiwasi wake kuhusu hali ya mvutano inayoendelea katika eneo la Magharibi mwa Asia na kusema: Iran ina nafasi chanya katika matukio ya eneo hilo na inafanya jitihada za kuimarisha utulivu na usalama.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema hayo kutokana na wasiwasi wa ongezeko la mivutano katika eneo la Magharibi mwa Asia baada ya kushadidi mashambulizi ya Israel dhidi ya watu wa Gaza na uungaji mkono wa Marekani kwa Tel Aviv. Amesema: Kwa kuzingatia nafasi chanya ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika matukio ya kanda ya Asia Magharibi, tunaiomba Tehran ifanye kila iwezalo kuzuia kuenea kwa mivutano katika eneo hilo.
Guterres amesisitiza kuwa: "Sisi sote lazima tufanye kila tuwezalo kurejesha utulivu na kupunguza hali ya wasiwasi katika eneo la Asia Magharibi na Bahari ya Shamu."
Utawala haramu wa Israel umeendeleza mashambulizi na mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza kwa miezi kadhaa sasa ukisaidiwa na nchi za Magharibi hususan Marekani.
Mashambulizi hayo ya Israel yameua zaidi ya watu 28,000 kufikia sasa, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto.