Feb 12, 2024 04:38 UTC
  • Taasisi ya utafiti Ujerumani yamfuta kazi profesa kwa kuitetea Palestina

Taasisi moja mashuhuri ya utafiti nchini Ujerumani imempiga kalamu nyekundu profesa wa anthropolojia anayeiunga mkono Palestina, baada ya msomi huyo kukosoa mashambulizi yanayoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Kanali ya Press TV imeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, Taasisi ya Utafiti ya Max Planck Society imevunja mkataba wake na mwanaakademia mtajika Ghassan Hage, kutokana na machapisho yake kadhaa katika mitandao ya kijamii ambayo eti hayaendani na 'thamani za kijamii'.

Taasisi hiyo mashuhuri ya utafiti ya Ujerumani imedai katika taarifa kuwa: Ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya Uislamu, chuki dhidi ya Mayahudi, kubaguana, uchochezi na chuki hazina nafasi katika taasisi ya Max Planck Society.

Profesa huyo wa Chuo Kikuu cha Melbourne mwenye uraia pacha wa Lebanon na Australia amelaani vikali uamuzi wa Taasisi ya Utafiti ya Max Planck Society wa kumfukuza kazi, kutokana na hatua yake ya kutumia uhuru wake wa kujieleza kukosoa jinai za Israel huko Gaza.

Chuki dhidi ya Uislamu zimeongezeka Ujerumani

Kwa mujibu wa jumuiya ya kiraia ya Turkish-Islamic Union (DITIB), hisia za chuki dhidi ya Uislamu, Waislamu na matukufu yao zimeogezeka kwa kiwango cha kutisha nchini Ujerumani, tangu utawala haramu wa Israel ulipoanzisha mashambulio yake ya kinyama dhidi ya Wapalestina wa Gaza mnamo Oktoba 7 mwaka uliopita 2023.

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya profesa wa sosholojia aliyefukuzwa kazi na Chuo Kikuu cha Bristol nchini Uingereza kutokana na maoni yake dhidi ya Wazayuni kushinda uamuzi wa kihistoria wa Mahakama ya Ajira, ambayo iliamua kwamba alibaguliwa kwa sababu ya itikadi zake.

Profesa David Miller alifutwa kazi na Chuo Kikuu cha Bristol mnamo Oktoba 2021 baada ya kutoa taarifa kuhusu nafasi na harakati ya Kizayuni katika kukuza chuki dhidi ya Uislamu.

Tags