Feb 12, 2024 07:33 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Februari 12

Natumai u mzima wa afya mpenzi msikilizaji popote uliopo. Karibu tuangazie japo kwa mukhtasari baadhi ya matukio yaliyotikisa viwanja mbalimbali, kitaifa, kieneo na kimataifa.

Kombe la Asia; Qatar bingwa baada ya kuinyuka Jordan

Timu ya taifa ya soka ya Qatar ndiyo wafalme wa soka barani Asia. Ndivyo unavyoweza kusema kwa ufupi baada ya kufikia tamati fainali za Kombe la Mataifa ya Asia. Siku ya Jumamosi, Qatar ilishuka dimbani kuvaana na Jordan katika ngoma ya fainali ya Kombe la Mataifa ya Asia na kuambulia ushindi wa mabao 3-1. Kwenye mchuano huo uliopigwa katika Uwanja wa Lusail, kusini mwa Manispaa ya Al Daayen, wenyeji licha ya kuupigia nyumbani walisindwa kuutawala mchezo na kuishia kufunga mabao yote kupitia mikwaju ya penati. Walitangulia kuona lango la wageni dakika 22 baada ya kuanza ngoma, kupitia goli la mshambuliaji nyota, Akram Afif ambaye aliongeza la pili kunako dakika ya 73, dakika 6 baada ya Jordan kusawazisha mambo. Afif mwenye umri miaka 26 alilizamisha kabisa jahazi la wenyeji kupitia baada ya kuvurumisha wavuni penati nyingine katika dakika za majeruhi, na kuwahakikishia wenyeji kuwa wanalihifadhi kombe, mbali na yeye binafsi kufunga mabao 3 ya hatrick kwenye mchuano huo.

Iran baada ya kunyukwa na wenyeji Qatar

 

Mabingwa hao watetezi walitinga fainali baada ya kuitandika Iran mabao 3-2 katika mchezo wa nusu fainali ya kukata na shoka iliyopigwa katika Uwanja wa al-Thumama jijini Doha. Iran walikuwa wa kwanza kutangulia kwa goli la mkasi la mshambuliaji nyota Sardar Azmoum, dakika nne baada ya kupulizwa kipyenga cha kuanza mchezo. Dakika 13 baadaye, nyota Akram Afifi alimuandalia pasi safi Jassem Gaber aliyewasawazishia wenyeji kabla a Afifi huyo kuongeza la pili kabla ya kumalizika kipindi cha kwanza. Alireza Jahanbakhsh aliwasawazishia Wairani kwa goli la dakika 51 kwa shuti akiwa ndani ya sanduka la hatari. Hata hivyo mambo yalizidi kuwaendeea segemnege Wairani baada ya Shoja Khalilzadeh kulimwa kadi nyekundu katika dakika za majeruhi. Almoez Ali alilazamisha jahazi la wageni kwa goli la ushindi kunako dakika ya 82 ya mchezo. Jordan ilitinga fainali baada ya kuisasambua Korea Kusini mabao 2-0.

Katika hatua nyingine, Shirikisho la Soka la Iran limesema litarefusha mkataba wa mkufunzi wa timu ya taifa ya kandanda ya Jamhuri ya Kiislamu, Amir Ghalenoei mpaka mwishoni mwa fainali za Kombe la Dunia la FIFA la 2026. Kocha mwenye umri wa miaka 60 alitangaza kuwa Mkfunzi Mkuu wa Iran mnamo Machi mwaka jana 2023.

Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON); Ivory Coast kidedea

Uwanja wa Alassane Outtara siku ya Jumapili jijini Abidjan ulitifua mavumbi na kuroroma moto mkali wakati wa fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) iliyowakutanisha wenyeji Ivory Coast na Nigeria. Wachezaji wa Kodivaa wakicheza mbele ya Rais wao Alassane Outtara, Rais wa Shirikisho la Soka Duniani FIFA, Giani Infantino, Rais wa Shirikisho la Soka Afrika CAF, Patrice Motsepe na mashabiki zaidi ya 60,000, walicheza kufa kupona na kuambulia ushindi wa mabao 2-1.

Wachezaji wa Kodivaa wakilibusu Kombe la Mataifa ya Afrika

 

Super Eagles walitangulia kuona lango la wenyeji kupitia goli la William Troost-Ekong dakika 38 baada ya kupupizwa kipyenga cha kuanza ngoma. Na kwa kuwa kutangulia sio kufika, chambelecho, wenyeji walijizoa zoa katika kipindi cha pili na kusawazisha mambo kupitia bao la Frank Kessie kunako dakika ya 62 ya mchezo. Ndovu hao walizidisha kasi baada ya goli hilo na kupata la ushindi katika dakika ya 81 kupitia Sebastien Haller.

Nigeria walisherehekea kufika fainali ya AFCON kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 11, baada ya kuizima Afrika Kusini kwa njia ya penalti mabao 4-2 katika nusu-fainali ya kwanza Jumatano. Cote d’Ivoire nao walitinga fainali baada ya kuinyamazisha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa mabao 2-1 katika nusu-fainali ya pili. Afrika Kusini na DR Congo zilivaana kutafuta mshindi wa medali ya shaba Jumamosi, ambapo vijana wa Bafana Bafana waliambulia ushindi japo kwa mbinde kupitia mikwaju ya penati. Hii ni baada ya kuhemeshwa na Batoto ba Kongo, na dakika za ada na nyongeza kumalizika kwa timu hizo kutoa sare tasa. Afrika Kusini walimaliza wa tatu kwa kutikisa nyavu mara 6, huku DRC ikitikiza mara 5.

Dondoo za Hapa na Pale

Shirikisho la Soka la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limelitaka Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kusitisha shughuli zote za soka za utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na utawala huo kutenda jinai huko Gaza. Katika barua yake kwa FIFA na mashirika ambayo ni wanachama wake, Shirikisho la Soka la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limesema: Kutokana na hatua zisizo za kibinadamu na jinai zinazofanywa na utawala haramu wa Israel huko Palestina hususan mauaji ya umati dhidi ya raia katika Ukanda wa Gaza Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) linapaswa kufungia shughuli zote za soka za utawala haramu wa Israel.

Jinai za Wazayuni Gaza

 

Sehemu moja ya barua ya Shirikisho la Soka la  Iran inasema, hatua ya FIFA inaweza kuzuia kuendelea jinai hizo zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Palestina na kutoa msaada wa chakula, maji ya kunywa, huduma za tiba na dawa kwa watu wasio na hatia na raia wa kawaida.

Wakati huo huo, Muungano wa Mashirikisho ya Soka ya Ulaya (UEFA) umekosolewa vikali na watumiaji wa mitandao ya kijamii baada ya kudai kuwa “haina nia” ya kuiondoa Israel nje ya michuano ya Ubingwa wa Uropa kutokana na jinai za utawala huo katika Ukanda wa Gaza. Katibu Mkuu wa bodi ya UEFA, Theodore Theodoridis, alikataa kata kata kuipiga marufuku Israel baada ya kundi la Vyama vya Soka vya Mashariki ya Kati kutaka utawala huo pandikizi ufurushwe kwenye mashindano ya dunia kutokana na vita vinavyoendelea Gaza. Hii ni katika hali ambayo, hapo awali Aleksander Ceferin, Rais wa UEFA aliiambia Telegraph Sports kuwa, kushiriki Israel na Ukraine kwenye mechi za EURO 2024 kunaweza kuwa tishio la usalama kwa mashindano hayo ya kieneo yanayotazamiwa kufanyika katika msimu ujao wa joto kali nchini Ujerumani. Rais wa UEFA alitoa indhari hiyo katika hali ambayo, chuki dhidi ya Wazayuni zimeongezeka kote duniani kufuatia vita vya utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza. Mapema mwezi huu wa Februari, Shirikisho la Soka la Asia Magharibi (WAFF) lilitoa mwito wa kusimamishwa utawala wa Israel katika mashindano na shughuli zote zinazohusiana na mpira wa miguu duniani, madhali Tel Aviv inaendeleza vita vya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza. Rais wa shirikisho hilo, Mwanamfalme Ali bin Hussein alitoa mwito huo katika barua ya wazi aliyoituma kwa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), mashirikisho ya kandanda na kwa wanachama wa vyama vya mchezo huo kote duniani.

Katika habari ya tanzia, ulimwengu wa riadha unaomboleza kifo cha mwanariadha nyota wa Kenya, Kelvin Kiptum aliyekuwa na umri wa miaka 24. Kiptum ambaye ni mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za marathon kwa upande wa wanaume, aliaga dunia Jumapili usiku katika ajali iliyohusisha gari lake pekee katika eneo la Kaptagat, katika barabara ya Elgeyo Maraktwet kueleke Ravine, eneo la Bonde la Ufa. Aidha mkufunzi wake Mnyarwanda, Garvis Hazikimana ambaye alikuwa kwenye gari hilo amepoteza maisha.

Mwendazake Kelvin Kiptum katika ubora wake

 

Na kwenye Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza, klabu ya Arsenal siku ya Jumapili ilijiongezea alama 3 muhimu baada ya kuigeuza West Ham kichwa cha mwenda wazimu na kuilima mabao 6-0. Gunners sasa wamefikisha alama 52 sawa na Man City, wakiwa katika nafasi ya 3 kwenye msimamo wa EPL. City hiyo siku ya Jumamosi iliizaba Everton mabao 2-0, huku watani wao wa jadi, Man United wakiilaza Aston Villa mabao 2-1. Liverpool ambao wametuama kileleni mwa jedwali la ligi wakiwa na alama 54, wikendi waliiadhibu Burnley mabao 3-1.

………………TAMATI……………..

 

Tags