Apr 18, 2024 05:49 UTC
  • Borrell: Ukraine isiombe kupewa msaada na Magharibi kama iliopewa Israel katika shambulio la Iran

Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema, Ukraine haipaswi kuomba msaada wa aina ile ile ambayo nchi za Magharibi zilitoa kwa Israel wakati wa shambulio la kijeshi la Iran kwa sababu hali hizo mbili haziwezi kulinganishwa.

Itakumbukwa kuwa tawala za Magharibi za Marekani, Uingereza na Ufaransa zilitangaza kuwa zilishirikiana na Jeshi la Ulinzi la utawala wa Kizayuni wa Israel (IDF) siku ya Jumamosi kuangusha baadhi ya makombora na ndege zisizo na rubani za Iran zilizokuwa zikielekea kwenye vituo vya kijeshi vya utawala wa Tel Aviv. Tokea lilipotolewa tangazo hilo, Rais wa Ukraine Vladimir Zelensky amekuwa akitoa wito kwa Washington na washirika wake ziifanyie vivyo hivyo nchi yake.

Katika kulipinga ombi hilo, Borrell ameeleza kwamba, "mashambulizi ya Iran yalifanywa kupitia juu ya vituo vya anga vya majeshi ya Ufaransa, Marekani, Uingereza na Jordan. Yamepita juu ya vituo vyao, kwa hivyo zilichukua hatua za kujilinda".

Zelensky

Ama kuhusiana na kadhia ya Kiev, Mkuu wa Sera za Nje wa EU ameseme: "hakuna vituo vya anga vya Uingereza au Marekani, na zaidi vya Jordan bila shaka, kwenye ardhi ya Ukraine au katika eneo yanakopita juu yake makombora ya Russia. Kwa hiyo, haliwezi kutolewa jibu kwa sababu hali zenyewe haziko sawa”.

Alipoulizwa na waandishi wa habari kama Umoja wa Ulaya kama taasisi ulishiriki katika kuulinda utawala wa Kizayuni na mashambulio ya Iran, Borrell amesema, umoja huo haukuhusika moja kwa moja, kwa sababu sio serikali na hauna jeshi, lakini baadhi ya wanachama wake walishiriki katika kufanya hivyo.../

 

Tags