Apr 25, 2024 02:32 UTC
  •  Kamina Johnson Smith
    Kamina Johnson Smith

Jamaica inasema imeamua kuitambua rasmi Palestina kama taifa huku kukiwa na wasiwasi wa muda mrefu juu ya vita vya Israel vinavyoendelea katika Ukanda wa Gaza na mzozo mbaya wa binadamu katika eneo hilo lililozingirwa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamaica, Kamina Johnson Smith, amethibitisha uamuzi huo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, akisisitiza kwamba hatua hiyo inaambatana na "dhamira imara" ya nchi yake kwa kanuni za Mkataba wa Umoja wa Mataifa, ambao unalenga kukuza kuheshimiana, kuishi pamoja kwa amani na haki ya kujitawala. Amesema: "Kwa kutambua Taifa la Palestina, Jamaica inaimarisha utetezi wake kuelekea suluhisho la amani."

Smith aliendelea kusema kuwa Jamaica inaendelea kuunga mkono kile kinachoitwa suluhisho la serikali mbili kama chaguo pekee linalowezekana kutatua mzozo wa muda mrefu wa Israeli na Palestina.

Pia amesema kuwa serikali ya nchi yake inasisitiza uungaji mkono wake kwa mazungumzo ya kidiplomasia badala ya hatua za kijeshi kama ufunguo wa kusuluhisha mzozo huo.

Waziri wa mambo ya nje wa Jamaica alisisitiza zaidi uungaji mkono wa nchi yake kwa usitishaji mapigano mara moja huko Gaza na kuongeza upatikanaji wa misaada ya kibinadamu, pamoja na amani ya kudumu katika eneo hilo.

Kwa hatua hii, Jamaica sasa inaungana na mataifa mengine 140 wanachama wa Umoja wa Mataifa katika kutetea suluhu la mataifa mawili katika mzozo wa Israel na Palestina.

Uamuzi wa Jamaca unakuja baada ya Barbados kutangaza uamuzi wake wa kuitambua rasmi Palestina kama taifa huru, na hivyo kujiunga na nchi 11 wa Jumuiya ya Karibea (CARICOM) ambazo zimeitambua.