Apr 25, 2024 02:43 UTC
  • Umaarufu wa Marekani barani Afrika waporomoka, China na Russia zavutia Waafrika wengi

Utafiti wa hivi karibuni katika zaidi ya nchi 130 uliofanywa na shirika la uchunguzi wa maoni la Marekani la Gallup umebaini kuwa umashuhuri wa Marekani umeshuka katika nchi nyingi za bara Afrika.

Utafiti huo ulifanywa katika nchi 36 za Afrika (yaani, karibu 66% ya nchi za bara hilo) ambapo waliohojiwa waliulizwa swali moja: "Je, unaidhinisha au unakataa utendaji kazi wa uongozi wa China, Russia au Marekani?

Umaarufu wa Marekani ulipungua kwa kiasi kikubwa katika mataifa matatu: Uganda, Gambia na Kenya (yaani kwa asilimia 29, 21 na 14 mtawalia). Umaarufu wa Marekani ulikuwa mdogo zaidi Libya na Somalia yaani 23% na 25%, mtawalia.

Kwa ujumla umaarufu wa China barani Afrika uko katika  58%  na Russia asilimia 42. Ingawa Umaarufu wa Marekani barani Afrika sasa ni asilimia 56, lakini kiwango hicho kimeshuka kwa kiwango kikubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Sababu ya kuongezeka kwa idhini ya Russia barani Afrika inaweza kuwa kwamba Moscow inaweza kukidhi mahitaji makubwa ya usalama ya bara hilo kupitia uuzaji wa silaha zinazohitajika kukabiliana na changamoto zilizopo.

 Kwa kuongezea, Russia inasaidia Afrika kutoa mafunzo ya ustadi wa kijeshi. Aidha China nayo imepata umaarufu barani Afrika kwa kulisaidia bara hilo katika miradi yake muhimu ya maendeleo na hivyo kuleta mabadiliko makubwa barani humo.