Apr 25, 2024 07:30 UTC
  • Amnesty International: Haki za binadamu duniani zingali zinakiukwa

Shirika la Kimataifa la Msamaha Duniani la Amnesty International limetangaza kuwa, haki za binadamu zingali zinakabiliwa na tishio kubwa katika maeneo mbalimbali duniani.

Ripoti ya shirika hilo la haki za binadamu inaonyesha kuwa, haki za binadamu zinazidi kukiukwa duniani kote na hali imezidi kuwa mbaya kwa miongo kadhaa sasa.

Hayo yamo katika ripoti ya kila mwaka iliyotolewa shirika la Amnesty International ambayo limeangazia migogoro ya Gaza na Ukraine pamoja na kuenea kwa tawala za kimabavu ambazo zinaharibu utaratibu wa kimataifa kwa kukiuka sheria za kimataifa na kutojali haki za kimsingi.

Katibu Mkuu wa shirika hilo Agnès Callamard ameashiria kuongezeka kwa migogoro ya silaha, Gaza, Ukraine na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu huko Sudan, Ethiopia na Myanmar akihoji kuwa utaratibu wa kimataifa unaotegemea kanuni uko katika hatari ya kuangamizwa.

 

Miongoni mwa mambo mengine, ripoti hiyo imekosoa vikali pia hatua ya Marekani ya kutumia kura yake ya turufu na hivyo kukwamisha juhudi za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa miezi kadhaa kuhusu azimio la kusitisha hujuma na mashambulio ya kinyama ya utawala ghasibu wa Israel katika Ukanda wa Gaza.

Ripoti ya Amnesty International inatolewa katika hali ambayo, madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani yameendelea kulaumiwa na walimwengu kutokana na hatua yao ya kuukingia kifua utawala dhalimu wa Israel sambamba na kuendelea kuupatia misaada ya silaha licha ya utawala huo kutenda jinai za kutisha huko Palestina hususan katika Ukanda wa Gaza.