Borrell: Nchi 4 za Ulaya kulitambua taifa la Palestina
(last modified Sat, 11 May 2024 07:58:20 GMT )
May 11, 2024 07:58 UTC
  • Borrell: Nchi 4 za Ulaya kulitambua taifa la Palestina

Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya amethibitisha kuwa nchi nne za Ulaya zitaitambua Palestina kama taifa huru.

Joseph Borrell alieleza hayo jana Ijumaa kwenye mahojiano aliyofanyiwa na vyombo vya habari vya Uhispania na kuongeza kuwa, nchi hizo wanachama wa EU ambazo zimetangaza kuwa zitalitambua taifa huru la Palestina ni Uhispania, Ireland, Slovenia, na Malta.

Borrell ambaye amekuwa akikosoa ukatili na mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanywa na utawala ghasibu wa Isarel dhidi ya watu wa Gaza huko Palestina amedokeza kuwa, yumkini Ubelgiji na nchi nchi nyingine kadhaa za Ulaya zikafuata mkumbo huo wa kulitambua taifa la Palestina.

Mwezi uliopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ireland, Micheál Martin alisema kuwa haikubaliki hata kidogo kukwamishwa na kucheleweshwa kutambuliwa nchi huru ya Palestina na kuongeza kwamba, hakuna kitu kinachoweza kuizuia nchi yake kutambua uwepo wa nchi huru ya Palestina.

Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Joseph Borrell

Aidha serikali ya Uhispania ilitangaza karibuni kwamba Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Pedro Sanchez atakutana na baadhi ya viongozi wenzake katika Umoja wa Ulaya kujaribu kuunga mkono suala la kutambuliwa rasmi taifa la Palestina.

Siku chache zilizopita, Bahamas ilitangaza rasmi kuwa inaitambua rasmi Palestina kama nchi. Nchi  nyingine iliyounga mkono kutambuliwa kwa taifa la Palestina katika wiki za hivi karibuni ni "Trinidad na Tobago" inayopatikana katika Bahari ya Caribbean huko kaskazini mwa Amerika ya Kusini. Aidha mwezi uliopita, Jamaica na Barbados pia zilitangaza kuwa zinalitambua taifa la Palestina. 

 

Tags