China na Marekani zatunishiana misuli juu ya Bahari ya China Kusini
China imeionya Marekani na waitifaki wake katika eneo dhidi ya kugeuza kadhia ya Bahari ya China Kusini kuchochea taharuki na vita.
Liu Zhenmin, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa China amesema Beijing inatumai kuwa, baada ya uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro, Marekani na waitifaki wake hazitalitumia suala hilo kuchochea vita na uhasama dhidi ya Beijing.
Matamshi hayo yamejiri siku moja baada ya mahakama hiyo ya kusuluhisha migogoro iliyoko mjini Hague nchini Uholanzi kupitisha uamuzi kuwa, China imehujumu uhuru wa kujitawala wa Ufilipino sambamba na kuchafua mazingira katika ardhi ya nchi hiyo, kwa kujenga kisiwa bandia katika maji hayo yanayozozaniwa.
Hata hivyo serikali ya Beijing imeutaja uamuzi huo kuwa hauna mantiki na ni kupoteza wakati; na kusisitiza kuwa China ina haki ya kutengeneza mifumo yake ya ulinzi wa anga katika Bahari ya China Kusini.
China inasisitiza kuwa, eneo la kistrataji la Bahari ya China Kusini ni milki yake, licha ya kugombaniwa na Ufilipino, Taiwan, Brunei, Vietnam na Malaysia huku ikiituhumu serikali ya Washington kuwa inaingilia masuala ya ndani ya nchi za eneo na kuchochea taharuki kwa makusudi.