Serikali ya Uingereza yatoa mwito wa kusitishwa haraka vita vya Gaza
David Lammy, Waziri mpya wa Mashauri ya Kigeni wa Uingereza ametoa wito wa kusitishwa mara moja vita katika Ukanda wa Gaza.
Katika taarifa yake ya kwanza kuhusu uvamizi wa Israel dhidi ya Gaza baada ya kuchukua wadhifa wa Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Lammy amesema, atafanya kila awezalo kuhakikisha vita vinasitishwa huko Gaza.
Lammy amesema atafanya kazi kuunga mkono usitishaji vita wa mara moja huko Gaza na kuachiliwa kwa mateka," na kuongeza, "nitafanya kila niwezalo kumsaidia Rais wa Marekani Joe Biden kufikia usitishaji wa mapigano.
Serikali mpya chini ya Waziri Mkuu mpya Keir Starmer imeundwa baada ya kufanyika uchaguzi siku ya Alkhamis. Chama cha Labour cha Uingereza kimepata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa Bunge uliofanyika jana Alhamisi, na kuhitimisha miaka 14 ya utawala wa Conservative, na hivyo kumfungulia milango kiongozi wake, Keir Starmer katika Downing Street.
Kulingana na matokeo ya uchaguzi huo yaliyochapishwa na televisheni ya Uingereza, chama cha Labour (katikati-kushoto) kitapata viti 410 kati ya 650 vya Bunge, kikiwatimulia kivumbi Wahafidhina, ambao watapata viti 131. Matokeo hayo ya viti vya chama tawala cha Conservative ndiyo mabaya zaidi tangu mwanzo wa karne ya 20.
Badhi ya wachambulizi wa mambo wanasema, wapiga kura wa Uingereza wamekiadhibu chama tawala cha Conservative kutokana na mgogoro wa gharama ya juu ya maisha, na siasa zake za masuala ya kigeni ikiwa ni pamoja na kuunga mkono kibubusa mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel katika Ukanda wa Gaza.