Afisa wa Marekani: Vita vya Hamas huko Gaza vinawahamasisha wengi
(last modified Sun, 07 Jul 2024 02:21:35 GMT )
Jul 07, 2024 02:21 UTC
  • Afisa wa Marekani: Vita vya Hamas huko Gaza vinawahamasisha wengi

Afisa wa Marekani amesema kuwa, shambulio la Hamas la tarehe 7 Oktoba dhidi ya Israel lilikuwa na litaendelea kuwa tukio la vizazi mbalimbali litakalotumiwa na makundi yenye silaha katika Mashariki ya Kati na duniani kote kama fursa ya kusajili wapiganaji.

 Gazeti la Washington Post lilimnukuu Brett M. Holmgren, Msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani katika Masuala ya Ujasusi akisisitiza kwamba vita vinavyoendeshwa na Hamas huko Gaza vinawatia moyo wengi, hususan waliokasirishwa na misaada ya Marekani kwa Israel.

Holmgren amesisitiza kwamba kuongezeka kwa hasira za walimwengu dhidi ya Marekani kutokana na misaada na uungaji mkono wake wa kijeshi kwa Israel sambamba na ongezeko la mauaji ya raia huko Gaza ni ukweli unaohisika kwa watu wote, na kwamba uungaji mkono huu unaibua chuki dhidi ya nchi yake.

Gaza

Hapo awali, gazeti la Washington Post lilinukuu ripoti ya kamati ya wataalamu huru inayojumuisha maafisa wa zamani wa Marekani, na kuhitimisha kwamba kuendelea uungaji mkono na misaada ya Washington kwa vita vya Israel dhidi ya watu wa Gaza kunadhoofisha uaminifu serikali ya Washington kwa watu.

Ripoti hiyo imeongeza kuwa, uuzaji wa silaha wa Rais wa Marekani Joe Biden kwa Israel unakiuka mipaka ya sheria, ikibainisha kuwa jeshi la Israel linapuuza sheria za kimataifa za kibinadamu, katika utumiaji wa silaha za Marekani huko Palestina.

Haya yanajiri huku wanajeshi wa Israel wakiendeleza mauaji ya kimbari Ukanda wa Gaza na hadi sasa zaidi ya Wapalestina 125,000 wameuawa shahidi au kujeruhiwa, wengi wao wakiwa watoto na wanawake, na zaidi ya 10,000 hawajulikani walipo.