Starmer: Siko tayari kuendeleza mpango wa kuwafukuza wahamiaji na kuwapeleka Rwanda
-
Keir Starmer
Waziri Mkuu mpya wa Uingereza, Keir Starmer, ametangaza kuwa "hayuko tayari" kuendeleza mpango mkuu wa serikali ya awali ya kihafidhina kuwafukuza wahamiaji na kuwapeleka Rwanda.
Starmer alisema jana - katika mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari - kwamba "Mpango wa Rwanda ulikufa na kuzikwa kabla haujaanza."
Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Rishi Sunak alikuwa akisisitiza juu ya mpango wake wa "kusimamisha boti" zinazovuka mfereji wa maji unaotenganisha Uingereza na Ufaransa na kusukuma mbele mpango wenye utata wa kuwafukuza na kuwapeleka Rwanda licha ya upinzani mkubwa wa makundi ya haki za binadamu na maamuzi ya mahakama, lakini chama cha Labour kiliahidi kwamba kitaweka kando mpango huo.
Starmer alisema hapo awali kuwa sera ya Sunak haikuwa ufumbuzi wala haina thamani yoyote, na kuahidi kushughulikia suala hilo "kimsingi" kwa kumaliza kabisa magenge yanayosafirisha watu.
Ni vyema kutambua kwamba Wzara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza ilisema mwezi uliopita kwamba inakadiriwa watu 12,313 wamevuka mpaka wa maji na kuingia Uingereza mwaka huu, ongezeko la 18% katika kipindi kama hicho mwaka jana.