Msimamo wa Erdoğan kuhusu ushirikiano wa NATO na utawala wa Kizayuni
Rais wa Uturuki amesema kuwa, ushirikiano wa Shirika la la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) na utawala wa Kizayuni wa Israel hauwezi kuendelea kwa sababu utawala huo ghasibu unakiuka thamani na maadili ya kimsingi ya muungano huo.
Recep Tayyip Erdoğan ameyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari baada ya kushiriki katika mkutano wa NATO uliohudhuriwa pia na Ukraine mjini Washington Marekani. Rais wa Uturuki amesisitiza kuwa, Israel inawaua kwa umati Wapalestina huko Gaza. Kabla ya Erdoğan, Uhispania pia ilitaka utendaji ulio sawa wa NATO kuhusiana na mgogoro wa wa Gaza kama ilivyo kwa Ukraine. Kwa sababu katika rasimu ya azimio la mwisho la mkutano wa kilele wa wakuuu wa NATO huko Washington, hakukutajwa hata neno moja kuhusu Gaza.
Ali Nikmanesh mweledi wa masuala ya kisiaasa anasema: "Shirika la NATO na nchi za Magharibi kwa ujumla siku zote huwa na mtazamo wa kindumakuwili kuhusiana na matukio ya kimataifa, jambo ambalo limedhihirika wazi kabisa katika suala la Gaza. Kwa mtazamo wa baadhi ya nchi wanachama wa NATO, kama vile Uturuki na hata Uhispania, " shirika hili la kijeshi linaweza kwa kuchukua msimamo wa kimantiki, likapiga jeki juhudi za kumalizika kwa haraka kwa vita huko Gaza na Ukraine pia."
Kwa mujibu wa Rais wa Uturuki ni kuwa, Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala dhalimu wa Kizayuni ni tishio kwa usalama wa eneo zima kutokana na kuendeleza vita huko Gaza. Rais Erdogan amesisitiza katika mazungumzo yake yote na viongozi mbalimbali pambizoni mwa mkutano wa NATO kwamba, kuna ulazima wa kuzingatiwa majanga yanayoendelea katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu hususan Gaza.
Uturuki pamoja na nchi nyingine za Kiislamu ziliweka mashinikizo maradufu dhidi ya utawala vamizi wa Israel ili ukomeshe jinai zake huko Gaza. Lakini Netanyahu, akiungwa mkono kikamilifu na Marekani, sio tu kwamba hakubaliani na usitishaji vita huko Gaza, bali anaendelea na jinai zake, ambapo hivi karibuni alifanya jinai nyingine kwa kushambulia shule na kuua makumi ya wanafunzi.
Kwa muktadha huo na kama alivyosema Rais Erdoğan nchi yake imefungua kesi dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu mjini The Hague pamoja na Afrika Kusini. Licha ya kuwa, kushtakiwa Israel katika asasi za kimataifa ni hatua muhimu sana, lakini sambamba na hatua hiyo kuna haja ya kukatwa kikamilifu uhusiano wa kisiasa na kibiashara baina ya utawala huo dhalimu na mataifa ya Kiislamu. Hapana shaka kuwa, kufanya hivyo kuna ufanisi mkubwa na kunaweza kuwa dawa mujarabu ya kuulazimisha utawala huo unaoua watoto kukomesha na kusitisha vita vyake vcya kinyama huko katika Ukanda wa Gaza.
Licha ya mataifa ya Kiislamu kuchukia na kulaani jinai za utawala wa Kizayuni huko Gaza, lakini bado hakujaanzishwa muungano kamili baina ya nchi hizo ili kuulazimisha utawala wa Kizayuni kusimamisha vita huko Gaza.