Japan inatafakari kulitambua rasmi taifa huru la Palestina
(last modified Sun, 14 Jul 2024 06:48:58 GMT )
Jul 14, 2024 06:48 UTC
  • Japan inatafakari kulitambua rasmi taifa huru la Palestina

Serikali ya Japan imefichua kuwa, inatathmini kwa uzito mkubwa suala la kulitambua rasmi taifa huru la Palestina.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Yoko Kamikawa amesema kwamba, nchi hiyo inatafakari mpango wa kulitambua rasmi taifa huru la Palestina, kwa kuzingatia maendeleo ya kile kinachoitwa mchakato wa amani wa Asia Magharibi.

Akiongea katika mkutano wa kiuchumi mjini Tokyo, manadiplomasia huyo mkuu wa Japan, 71, amesema nchi yake 'inaelewa' azma ya Wapalestina ya kutaka kuwa na nchi huru, na kwamba inaunga mkono 'suluhisho la kuundwa madola mawili' kama suluhu ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa miongo kadhaa wa Palestina na Israel.

Kabla ya hapo, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu,  Ahmed Aboul Gheit akiziungumza mjini Tokyo katika Mkutano wa Tano wa Kiuchumi wa Japan na Waarabu, alitoa mwito kwa Japan kuitambua Palestina kama nchi huru.

Wajapan katika maandamano ya kuiunga mkono Palestina

Nchi mbali mbali duniani kama vile Armenia, Uhispania, Ireland na Norway hivi karibuni zilipasisha rasmi mpango wa kutambua rasmi Palestina; na hivyo kukaidi matakwa ya utawala haramu wa Israel ambao unapinga hatua kama hizo.

Aidha katika miezi ya karibuni, waungaji mkono wa Wapalestina wamekuwa wakilaani jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza kwa kufanya maandamano duniani kote, ikiwemo nchini Japan.