China: Tuko tayari kushirikiana na serikali ijayo ya Iran
(last modified Tue, 16 Jul 2024 07:18:54 GMT )
Jul 16, 2024 07:18 UTC
  • China: Tuko tayari kushirikiana na serikali ijayo ya Iran

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesema China inathamini uhusiano wake na Iran na iko tayari kushirikiana na serikali mpya ya Jamhuri ya Kiislamu ili kuendeleza ushirikiano wa kimkakati na wa kina kati ya pande mbili.

Sanjari na kupongeza makala iliyoandikwa hivi karibuni na Rais mteule wa Iran, Masoud Pezeshkian akieleza kuwa serikali yake itaimarisha uhusiano wa kirafiki na China, Lin Jian, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesema azma ya viongozi wa Beijing ya kuendeleza na kupanua ushirikiano wa pande mbili na Tehran katika nyanja tofauti ni kubwa.

Amesema, China inathamini ujumbe wa Rais mteule wa Iran, Masoud Pezeshkian juu ya uhusiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu na China na kuongeza kuwa, "Uhusiano wa kirafiki kati ya nchi zetu mbili ulianza karne nyingi zilizopita. Katika kipindi cha miaka 50 iliyopita, hasa tangu nchi hizi mbili zianzishe uhusiano wa kidiplomasia, mahusiano baina ya mataifa mawili yamekuwa na ukuaji mzuri na madhubuti."

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China ameeleza bayana kuwa, Iran na China zina uwezo mkubwa wa kuendeleza na kuimarisha uhusiano na kupanua wigo wa ushirikiano wao.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China 

Wiki iliyopita, Mohammad Mokhber, Kaimu Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Rais Xi Jinping wa China walikutana na kuzungumzia uhusiano wa pande mbili, pambizoni mwa Mkutano wa 24 wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai huko Astana, mji mkuu wa Kazakhstan.

Katika kipindi cha uongozi wa Shahidi Ebrahim Raisi, uhusiano wa Beijing na Tehran ulipiga hatua kubwa, na hivi sasa inaonekana kuna azma thabiti ya pande mbili kuendeleza mkondo huu ili kuhakikisha kwamba, unastawi zaidi kuliko hapo awali.

Tags