Marekani na Ujerumani; Wauzaji silaha wakuu kwa utawala katili wa Israeli
(last modified Sun, 21 Jul 2024 07:25:47 GMT )
Jul 21, 2024 07:25 UTC
  • Marekani na Ujerumani; Wauzaji silaha wakuu kwa utawala katili wa Israeli

Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI) imetangaza katika ripoti yake kwamba kati ya asilimia 99 ya silaha zilizoagizwa na utawala wa Israel unaofanya mauaji ya kimbari huko Ukanda wa Gaza kati ya mwaka 2019 na 2023, asilimia 69 ilitoka Marekani na asilimia nyingine 30 kutoka Ujerumani.

Kabla ya kuanza operesheni ya kimbunga cha Al-Aqsa tarehe 7, Oktoba mwaka jana na kufuatiwa na jinai za utawala wa Kizayuni katika ukanda huo, Washington ilikuwa ikiitumia Israel silaha zenye thamani ya wastani wa dola bilioni tatu kila mwaka, na pia katika miaka mitano iliyopita, utawala huo wa Kizayuni umepokea asilimia 3.6 ya silaha zote zinazouzwa nje na Marekani.

Kwa mujibu wa taasisi hiyo, Marekani ilituma maelfu ya silaha na makombora ya kisasa kwa utawala wa Kizayuni kufikia mwishoni mwa mwaka jana.

Marekani ndio muuzaji mkuu wa zana za mauaji ya umati kwa Wapalestina

Katika uwanja huo, mwaka jana, serikali ya Ujerumani ilitoa leseni ya kuuziwa utawala huo katili silaha zenye thamani ya Euro milioni 326.5.

Kwa mujibu wa ripoti hii, kufikia mwishoni mwa mwaka 2023, ni Euro milioni 38.5 tu za mauzo ya kijeshi kwa utawala wa Kizayuni ndizo ziliidhinishwa na serikali ya Ujerumani.

Baada ya Oktoba 7, 2023, tangu utawala huo katili uanzishe mashambulizi ya kinyama dhidi ya watu wa Palestina huko Ukanda wa Gaza, idadi hii imeongezeka maradufu, ambapo sasa uko katika nafasi ya saba kati ya wapokeaji wakuu wa teknolojia ya kijeshi ya Ujerumani.

Kutumwa silaha za Wajerumani kwenye ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo haramu wa Israel huko Palestina kumekosolewa mara nyingi na watu wanaowatetea watu madhulumu na wanaozingirwa na kuuawa kinyama katika ukanda huo.

Mapema mwaka huu, 2024 Kituo cha Ulaya cha Haki za Kikatiba na Kibinadamu (ECCHR) kiliwasilisha kesi mahakamani dhidi ya serikali ya Ujerumani katika mahakama ya Berlin ikiwa ni katika jaribio la kusitisha uuzaji wa silaha kwa utawala haramu wa Israel.