Ujerumani yakosolewa kwa kumfukuza mwanachuoni wa Kiislamu
(last modified Fri, 30 Aug 2024 02:42:26 GMT )
Aug 30, 2024 02:42 UTC
  • Ujerumani yakosolewa kwa kumfukuza mwanachuoni wa Kiislamu

Watumiaji wa mitandao ya kijamii wameikosoa vikali serikali ya Ujerumani kwa kumtimua nchini humo mwanachuoni mmoja mashuhuri wa Kiislamu.

Wiki tano baada ya Kituo cha Kislamu cha Hamburg (IZH) kupigwa marufuku baada ya kutuhumiwa kuwa inatoa mafunzo ya itikadi kali, mkuu wake wa zamani sasa ametakiwa kuondoka nchini Ujerumani.

Jana Alkhamisi, Mamlaka ya Ndani ya Hamburg ilitoa amri ya kurudishwa kwao Sheikh Mohammad Hadi Mofatteh, 57. Haikueleza iwapo Sheikh Mofatteh bado yupo nchini Ujerumani au la. Mamlka hiyo inamtaka msomi huyo wa Kiislamu aihame Ujerumani ndani ya siku 14, la sivyo atarudishwa katika nchi aliyotokea kwa gharama yake mwenyewe. Kulingana na mamlaka hiyo, anastahili kuondoka Ujerumani kufikia Septemba 11.

Aidha amepigwa marufuku ya kurudi Ujerumani au kuishi nchini humo na iwapo atafanya hivyo, huenda akafungwa jela kwa kipindi cha miaka mitatu.

Polisi ya Ujerumani walipovamia Kituo cha Kiislamu cha Hamburg

Wiki mbili zilizopita, Sekretarieti ya Umoja wa Mabunge ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ililaani kitendo cha kufungwa vituo vya Kiislamu nchini Ujerumani.

Ilisema hatua za serikali ya Berlin za kufunga vituo hivyo zinakinzana na misingi ya haki na uhuru wa binadamu, hasa uhuru wa dini na itikadi, uhuru wa maoni na uhuru wa watu binafsi.

Aidha Iran ililaani vikali hatua ya polisi ya Ujerumani ya kupiga marufuku Kituo cha Kiislamu cha Hamburg (IZH) na asasi zake tanzu, na kusema kwamba hatua hiyo inakiuka kanuni za kimsingi za uhuru wa kuabudu.