Mashirika ya haki za binadamu yataka UN 'iwalinde' mateka wa Kipalestina
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yametoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za haraka "kuwalinda watu walionyimwa uhuru wao" katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
Katika taarifa, mashirika 31 ya haki za binadamu yakiwemo Save the Children, Human Rights Watch na Oxfam yamezitaka nchi wanachama wa UN kuchukua hatua za kuhakikisha kwamba watoto na watu wazima wa Kipalestina wanaoshikiliwa mateka na Israel hawafanyiwi vitendo visivyo vya kiutu kama ilivyoainishwa na sheria ya kimataifa ya kibinadamu na haki za binadamu.
"Hii ni pamoja na kuhakikisha kwamba Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) inaruhusiwa bila vikwazo kuwafikia kwa wafungwa na mateka wote, kwa kiwango kamili kinachohitajika na sheria ya kimataifa ya kibinadamu," imesema taarifa hiyo.
Mashirika hayo pia yamesema kwamba, watoto wa Kipalestina waliokamatwa kiholela na kuzuiliwa na jeshi la Israel wanapaswa kuachiliwa "mara moja na bila masharti."
Taarifa hiyo ilionyesha kwamba watoto wa Kipalestina wanaoshikiliwa na jeshi la Israel wanaandamwa na ukandamizaji na unyanyasaji ulioratibiwa, huku ripoti za vitendo vya udhalilishaji, ikiwa ni pamoja na kuvuliwa nguo kwa lazima ili wapekuliwe, na kulazimishwa kuiga wanyama. Mashirika hayo yameongeza kuwa, "Hakuna mtoto anayepaswa kuwasiliana na mahakama ya kijeshi, au mahakama yoyote ambayo haina haki kamili ya kimsingi. Hakuna mtoto anayefaa kutekwa nyara.”
Kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za binadamu la B’Tselem, karibu Wapalestina 10,000 kwa sasa wanazuiliwa au wamefungwa jela kwa kile ambacho Israel inakitaja kuwa ni misingi ya "usalama", ambapo 1,761 kati yao wanatoka Ukanda wa Gaza.