Maandamano ya waungaji mkono Palestina katika siku ya uchaguzi Marekani
(last modified Wed, 06 Nov 2024 10:58:29 GMT )
Nov 06, 2024 10:58 UTC
  • Maandamano ya waungaji mkono Palestina katika siku ya uchaguzi Marekani

Sambamba na siku ya uchaguzi wa rais nchini Marekani, waungaji mkono wa Palestina wameandamana mjini New York kupinga sera ya serikali ya Marekani kuhusu Palestina.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Iran Press, wafuasi wa Palestina walianzisha maandamano yao kwa kukusanyika mbele ya ofisi ya Televisheni ya Fox News Jumanne jioni, saa za New York, na maandamano haya kuendelea hadi usiku wa manane.

Vikosi vya polisi vya Marekani, vilikabiliana na umati mkubwa wa waungaji mkono hao wa Palestina mjini New York.

Waandamanaji walisisitiza katika maandamano hayo kwamba  hakuna tofauti katika sera za Donald Trump na Kamla Harris dhidi ya Palestina na kwamba wawili hao ni wafuasi sugu wa utawala haramu wa Israel.

Waandamanaji hao walibeba bendera za Palestina huku wakichoma moto bendera za utawala wa Israel sambamba na kulaani jinai za utawala huo huko Gaza. 

Utawala haramu wa Israel, kwa himaya kamili ya Marekani umekuwa ukipuuza maazimio ya Umoja wa Mataifa na Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu ya kuutaka usitishe mauaji ya kimbari huko Gaza.

Uvamizi huo wa Israel umewaua zaidi ya Wapalestina 43,400 huko Gaza, wengi wao wakiwa wanawake na watoto. Mashambulizi hayo ya kiholela pia yamesababisha takriban watu milioni 2.3 kuwa wakimbizi wa ndani.