Mkutano wa UN kuhusu kuenea majangwa duniani umeanza Riyadh, Saudi Arabia
Wazungumzaji katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa kupambana na kuenea majangwa duniani COP16 unaoendelea nchini Saudi Arabia wametahadharisha kuwa hatua zinapasa kuchukuliwa ili kulinda uhai duniani.
Ibrahim Thiaw Naibu Katibu Mkuu na Katibu Mtendaji wa UNCCD amesema katika mkutano wa Umoja wa Mataifa wa COP16 huko Riyadh, kwamba mustakbali wa maisha yetu duniani utaamuliwa na namna tunavyosimamia na kutunza ardhi yetu.
Mkutano wa COP16 wa Riyadh umeanza tangu jana tarehe Pili na utaendelea hadi tarehe 13 mwezi huu wa Disemba chini ya kauli mbiu "Ardhi yetu, mustakbali wetu."
Mkutano wa Riyadh unafanyika lengo likiwa ni kuwakutanisha pamoja viongozi wa dunia, wataalamu na wawakilishi wa jamii kutoka pembe mbalimbali duniani ili kutafuta njia za kukabiliana na kuenea majangwa duniani.
Shirika la hali ya hewa la Umoja wa Mataifa liliripoti mwezi Oktoba kwamba mwaka 2023 ulikuwa mwaka wa ukame mkubwa kuwahi kushuhudiwa kwa zaidi ya miongo mitatu. Ukame huo uliathiri mito mingi duniani kutokana na joto kusababisha kukauka kwa mtiririko wa maji na kuchangia ukame wa muda mrefu katika baadhi ya maeneo duniani.