Wamagharibi na mchezo wa undumakuwili kuhusu jinai za Israel
https://parstoday.ir/sw/news/world-i120192-wamagharibi_na_mchezo_wa_undumakuwili_kuhusu_jinai_za_israel
Licha ya hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai dhidi ya viongozi wa utawala wa Kizayuni, mahakama ya Uholanzi imetupilia mbali kesi iliyowasilishwa kwa lengo la kuzuia kuuziwa silaha za nchi hiyo utawala ghasibu wa Israel.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Dec 15, 2024 23:09 UTC
  • Wamagharibi na mchezo wa undumakuwili kuhusu jinai za Israel

Licha ya hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai dhidi ya viongozi wa utawala wa Kizayuni, mahakama ya Uholanzi imetupilia mbali kesi iliyowasilishwa kwa lengo la kuzuia kuuziwa silaha za nchi hiyo utawala ghasibu wa Israel.

Mahakama hiyo imedai katika taarifa yake kwamba, hakuna sababu ya kupiga marufuku kabisa usafirishaji wa bidhaa za kijeshi na za madhumuni mawili kwa Israel. Matokeo yake, madai yote yanatupiliwa mbali.

Muungano wa makundi yanayounga mkono Palestina umesema kuwa, mamlaka za Uholanzi zimeshindwa kuzuia "mauaji ya halaiki" yanayofanywa na utawala wa Israel wakati wa mashambulizi yake ya kikatili huko Gaza. Wout Albers, mwanasheria anayetetea mashirika yasiyo ya kiserikali, alisema mahakamani: Israel ina hatia ya mauaji ya kimbari na ubaguzi wa rangi na inatumia silaha za Uholanzi katika vita vyake.

Hata hivyo wakili wa serikali ya Uholanzi Reimer Veldhius aliiambia mahakama kuwa Uholanzi imetumia sheria za Ulaya katika uuzaji wa silaha na kuiomba mahakama kutupilia mbali kesi hiyo, jambo ambalo mahakama ililikubali.

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC imetoa waranti wa kukamatwa waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na aliyekuwa waziri wa vita Yoav Gallant

 

Ingawa hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ilizifanya nchi nyingi duniani kuiwekea vikwazo vya silaha Israel, lakini washirika wa Israel kama Marekani na nchi nyingi za Ulaya ambazo ni wauzaji wakuu wa silaha kwa utawala wa Kizayuni, zimekataa kutekeleza hukumu hiyo.

Hii ni katika hali ambayo, ukubwa wa jinai za Israel dhidi ya Wapalestina ulipelekea suala la vikwazo vya silaha dhidi ya Israel kuwa ombi la kimataifa katika miezi kadhaa iliyopita.

Pia, nchi nyingi zimejiunga na kundi la nchi zinazounga mkono kesi ya Afrika Kusini dhidi ya utawala wa Kizayuni katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ.

Mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka jana 2023, Afrika Kusini iliwasilisha malalamiko katika Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu dhidi ya utawala wa Kizayuni kutokana na utawala huo kukiuka makubaliano ya kupigwa marufuku jinai za mauaji ya halaiki.

Mwezi uliopita, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ilitoa waranti wa kukamatwa waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na aliyekuwa waziri wa vita Yoav Gallant baada ya kuwafungulia mashtaka ya kutenda jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu huko Gaza, ambako utawala wa Kizayuni umekuwa ukiendesha vita vya kinyama na kufanya mauaji ya kimbari tangu mwezi wa Oktoba mwaka jana.

Kuhusiana na hilo, New Gordon, profesa wa sheria za kimataifa katika Chuo Kikuu cha Malkia Mary cha London, alisema: Kwa kutoa hati ya kukamatwa kwa Netanyahu na Gallant kuhusiana na uhalifu wa kivita na jinai dhidi ya ubinadamu, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kwa hakika imezitaka nchi za Magharibi kuutazama upya aina ya mikataba  ya kibiashara na utawala wa Kizayuni  wa Israel hususan biashara inayohusiana na silaha, kwa sababu silaha zinazotolewa na nchi za Magharibi zinatumika kufanya jinai dhidi ya binadamu.

 

Pia, Eran Shamir Borer, mkurugenzi wa Kituo cha Usalama wa Taifa na Demokrasia katika Taasisi ya Demokrasia ya Israel, pia ameliambia gazeti la Kizayuni la Haaretz kwamba:

Uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC unaweza kusababisha nchi nyingi za magharibi kusitisha usafirishaji wa silaha hadi Tel Aviv. Afisa huyo anaeleza kuwa, katika kila mkataba, kifungu kinabainisha wazi kipengee kisemacho kwamba nchi haziwezi kupeleka silaha hizi kwa asasi ambayo inatumia kwa ajili ya ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu kama vile mkataba wa pande nne wa 1949 Geneva na protokali ziada za 1977.

Licha ya maamuzi hayo yote, usafirishaji wa silaha kuelekea Israel unaendelea. Ukweli ni kwamba, nchi za Magharibi kama vile Uholanzi, bila ya kujali nara zao zote za kibinadamu, bado zinazungumzia haki za binadamu katika nyuso mbili na kwa upande mwingine, zinaendelea kutoa uungaji mkono wa kisiasa na kijeshi kwa utawala wa Kizayuni wa Israel unaotekeleza jinai za kivita. Suala hili pia linaonyesha undumilakuwili wa Wamagharibi katika kutetea haki za binadamu.