Pakistan yakanusha madai ya Marekani kuhusu mpango wake wa makombora
Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan imepuuzilia mbali madai yaliyotolewa na afisa wa ngazi za juu wa Marekani kwamba mpango wa makombora ya balistiki ya Islamabad ni tishio kwa usalama wa Marekani na kusema madai hayo hayana msingi wala mantiki
Siku ya Alhamisi, Jon Finer, Naibu Mshauri wa Usalama wa Taifa wa utawala wa Biden, alidai kwamba mpango wa makombora wa Islamabad unaibua "maswali ya msingi" kuhusu nia yake.
Finer alisema: "Pakistan imeunda teknolojia ya kisasa zaidi ya makombora, kutoka kwa mifumo ya makombora ya masafa marefu hadi vifaa ambavyo vitawezesha majaribio ya injini kubwa zaidi za roketi."
Alisema Pakistan ikijiimarisha zaidi itaweza kulenga maeneo ya Asia Kusini na Marekani.
Alitoa kauli hiyo siku moja baada ya Washington kutangaza awamu mpya ya vikwazo kuhusiana na "vyombo vinne vinavyochangia programu ya makombora ya balistiki ya Pakistan."
Akijibu maswali ya vyombo vya habari kuhusu matamshi ya Finer na awamu mpya ya vikwazo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan, Mumtaz Zahra Baloch amesema Pakistan imehusishwa kimakosa na mataifa yanayotambulika kuwa wapinzani wa Marekani. Baloch amesema wasiwasi kuhusu mpango wa makombora ya balistiki ya Pakistani unakuzwa ili kuyumbisha zaidi uwiano wa kimkakati wa eneo hilo.
Ameashiria tofauti inayoonekana katika jinsi Marekani inavyoshughulikia uwezo wa makombora katika nchi jirani ya India.
Amesema kuwa uwezo wa makombora ya balistiki ya nchi yake umeundwa kutetea uhuru wake na kuhakikisha amani na utulivu katika Asia Kusini. Amesisitiza zaidi haki ya Pakistan ya kuendeleza na kustawisha uwezo wake wa ulinzi kama kizuizi dhidi ya vitisho vya kikanda.