Poland: Tutamkamata Netanyahu iwapo atahudhuria maadhimisho ya 80 ya kukombolewa Auschwitz
https://parstoday.ir/sw/news/world-i120496-poland_tutamkamata_netanyahu_iwapo_atahudhuria_maadhimisho_ya_80_ya_kukombolewa_auschwitz
Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu atakamatwa iwapo atahudhuria sherehe zitakazofanyika mwezi ujao nchini Poland za kuadhimisha miaka 80 ya kukombolewa mji wa Auschwitz. Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo mwanachama wa Umoja wa Ulaya Wladyslaw Bartoszewski katika mahojiano na gazeti la Rzeczpospolita.
(last modified 2024-12-23T02:57:55+00:00 )
Dec 23, 2024 02:57 UTC
  • Poland: Tutamkamata Netanyahu iwapo atahudhuria maadhimisho ya 80 ya kukombolewa Auschwitz

Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu atakamatwa iwapo atahudhuria sherehe zitakazofanyika mwezi ujao nchini Poland za kuadhimisha miaka 80 ya kukombolewa mji wa Auschwitz. Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo mwanachama wa Umoja wa Ulaya Wladyslaw Bartoszewski katika mahojiano na gazeti la Rzeczpospolita.

Mwanadiplomasia huyo mwandamizi wa Warsaw amebainisha kuwa Poland, ikiwa ni nchi iliyosaini Mkataba wa Roma, inawajibika kufuata maagizo ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC). Mwezi Novemba, ICC ilitoa hati za kukamatwa Netanyahu na aliyekuwa waziri wa vita wa utawala wa Kizayuni Yoav Gallant kwa kutuhumiwa kuhusika na jinai za kivita zilizofanywa na jeshi la Israel katika vita vya Ghaza.

Wakati nchi zote 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya ni wanachama wa Mkataba wa Roma na hivyo zinawajibika kutekeleza hati zilizotolewa na Mahakama ya Kimataita ya Jinai za kuwatia nguvuni Netanyahu na Gallant, misimamo ya nchi hizo kuhusiana na utekelezaji wa agizo hilo la ICC imetofautiana kati ya nchi na nchi. Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban amemwalika Netanyahu waziwazi kutembelea nchi hiyo akimhakikishia kwamba Hungary haitatekeleza agizo la kukamatwa kwake.

Kinyume chake, nchi kama Uhispania, Uholanzi, Ubelgiji, Ireland, Lithuania, na Slovenia zimeonyesha nia yao ya kutii maagizo ya ICC, bila kujali kinga ya kidiplomasia anayodaiwa kuwa nayo waziri mkuu huyo wa utawala wa Kizayuni.

Ufaransa, awali ilieleza nia yake ya kuheshimu na kuifanyia kazi hati iliyotolewa na Mahakama ya The Hague ya kumkamata Netanyahu lakini baadaye ikataja kisingizio cha kinga ya kidiplomasia kama hoja ya kutokuwa tayari kumkamata waziri mkuu huyo wa utawala wa Kizayuni.

Ikumbukwe kuwa, Auschwitz ilikuwa kambi ya mateso na mauaji ya utawala wa Kinazi wa Ujerumani katika Poland iliyokaliwa kwa mabavu wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Zaidi ya Wayahudi milioni 1.1 waliripotiwa kwamba waliuawa kwenye kambi hiyo pamoja na makumi ya maelfu ya watu wengine, wakiwemo wafungwa wa kivita wa Poland na wa Shirikisho la Kisovieti la Urusi.../