Ugaidi, chombo cha kisiasa cha nchi za Magharibi
Licha ya kupita siku kadhaa tangu tukio la watu kugongwa na gari katika soko la Krismasi la Magdeburg, Ujerumani, suala hili bado linagonga vichwa vya habari katika vyombo vya habari vya Magharibi. Makumi ya watu waliuawa auu kujeruhiwa katika tukio hilo.
Kansela wa Ujerumani, Olaf Schultz alitembelea eneo la tukio hilo kwa ajili ya kutoa mkono wa pole kwa waathiriwa. Ingawa imebainika kuwa mhusika wa tukio la Magdeburg alikuwa mtu anayepinga Uislamu, vyombo vya habari vya Magharibi vinajaribu kujikita zaidi kwenye utaifa na dini ya mhusika wa tukio hilo.
Katika matukio ya kigaidi yanayotokea katika nchi za Magharibi, mtuhumiwa nambari moja kabisa huwa Waislamu au raia kutoka nchi za Waislamu. Serikali, vyombo vya usalama na vyombo vya habari vya Magharibi pia vinajaribu kuhamishia matukio haya nje ya mipaka ya Ulaya, na suala hilo linageuka kuwa mjadala wa kupinga wahajiri na dhidi ya Uislamu katika ushindani baina ya vyama vya siasa. Hali hii imeonekana pia baada ya tukio la Magdeburg huko Ujerumani. Hata hivyo baadaye, ilibainika kuwa mhusika wa tukio hilo ni daktari Msaudi Arabia mwenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia na mwenye chuki dhidi ya Waislamu, ambaye alipewa hifadhi nchini Marekani. Ili kutumia tukio hili kwa madhumuni ya kisiasa na kipropaganda, mara hii wamejikita zaidi kwenye dini na uraia wake wa Saudia.
Jarida la Ujerumani Der Spiegel limeripoti kwamba mhalifu huyo ni daktari aliyebobea katika tiba ya kisaikolojia na anaunga mkono fikra za chama cha mrengo wa kulia cha Alternative for Germany.
Vilevile imethibitika kuiwa, anatafutwa na Saudi Arabia kwa tuhuma zinazohusiana na ugaidi na biashara ya binadamu inayohusisha watu binafsi kutoka Saudi Arabia na mataifa mengine ya Ghuba ya Uajemi kelekea kwenye nchi za Umoja wa Ulaya (EU).
Ujerumani ilikataa kumrejesha Saudi Arabia na badala yake ikampa hifadhi ya kisiasa mwaka 2006.
Wakati huu ambapo sababu na chachu ya tukio la Magdeburg bado haijabainika, vyombo vya habari vya Ujerumani na nchi nyingine za Magharibi vinasisitiza zaidi dini na Usaudia wake. Wapinga wahajiri na wanaopiga vita Uislamu nchini Ujerumani na nchi nyingine za Ulaya pia wanaliona tukio la Magdeburg kuwa ni uthibitisho wa sera zao za chuki dhidi ya wahajiri na Uislamu. Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orbán, amedai katika taarifa yake kwamba: Shambulio hilo ni matokeo ya uhamiaji haramu na kumiminika wahamiaji katika bara la Ulaya. Orbán amesema, tangu kuanza mgogoro wa wahajiri barani Ulaya tumekuwa tukishuhudia matukio ya aina hiyo mara kwa mara, na kusisitiza kwamba hapana shaka kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya wimbi la wahajiri hasa wahamiaji haramu bara la Ulaya, na kutokea kwa uhalifu huu.
Kutokana na sababu za kihistoria, kisiasa na kiuchumi, Ulaya imekuwa makimbilio ya sehemu kubwa ya wahamiaji kutoka Afrika na Magharibi na Kusini mwa Asia. Uhamiaji kuelekea barani Ulaya ulianza baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia na wakati wa wimbi la kupigania uhuru katika makoloni ya nchi za Ulaya baada ya Vita vya Pili vya Dunia. Katika miaka 80 iliyopita, mawimbi kadhaa ya kuhamia Ulaya yametokea sambamba na mabadiliko na matukio ya kikanda na kimataifa. Wazungu wamekuwa na mchango na nafasi ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja katika uhamiaji huo. Miongoni mwa mawimbi hayo ya uhamiaji kuelekea Ulaya ni wakimbizi waliokwenda barani humo kutoka Asia Magharibi, hasa Syria. Mgogoro huu uliibuliwa na nchi za Magharibi huko Syria tangu mwaka 2010, ambapo ziliifanya Syria kuwa uwanja wa makundi ya kitakfiri na kigaidi na kuwalazimisha zaidi ya nusu ya wakazi wa Syria kuwa wakimbizi. Baadhi ya wakimbizi hawa walikwenda Ulaya kwa ajili ya kutafuta maisha bora au kuokoa maisha yao.
Ili kuhadaa maoni ya umma, wakati huo nchi za Ulaya zilijumuisha baadhi ya makundi ya kigaidi na kitakfiri na viongozi wao katika orodha ya makundi ya kigaidi. Bali walikwenda mbali zaidi katika hadaa hiyo kwa kutenga zawadi ya kitita kikubwa cha fedha kwa mtu atakayesaidia kukamatwa baadhi ya viongozi wa makundi hayo. Mojawapo ya makundi hayo lilikuwa Tahrir al-Sham na kiongozi wake, Jolani, ambaye zilitengwa dola milioni kumi kwa ajili ya kichwa chake. Sasa, baada ya kuanguka utawala wa Bashar Assad, jumbe za kidiplomasia za Ulaya zimejipanga katika safu ya kukutana na Jolani na zinataka kuondoa majina yake na kundi lake katika orodha ya makundi ya kigaidi. Hii ni kwa sababu, maslahi yao sasa yanawatuma kufanya kazi na kundi hilo.
Kwa hakika ugaidi ni chombo na wenzo unaotumiwa na serikali za nchi za Magharibi kwa ajili ya kuendeleza sera zao ndani na nje ya mipaka ya Ulaya. Viongozi na wanasiasa wa nchi hizo hulitaja kila tukio linalojiri katika nchi za Ulaya kuwa ni la kigaidi, na awali ya yote, huwatuhumu Waislamu na wahajiri kuwa ndio wahusika wa matukio hayo.
Inatupasa kukumbusha hapa kuwa, muundo wa idadi ya watu katika nchi za Ulaya umebadilika. Wahamiaji na wahajiri sasa wanaunda jamii kubwa za waliowachache katika nchi nyingi za Ulaya, hasa katika nchi zenye watu wengi na wana mchango na nafasi si ndogo katika masuala ya kisayansi, kiuchumi, kijamii, utamaduni na michezo. Sera za serikali za Ulaya dhidi ya wahajiri na chuki dhidi ya Uislamu ni ishara ya kufeli sera ya tamaduni mseto barani Ulaya ambayo imekuwa ikipigiwa debe tangu baada ya vita vya Pili vya Dunia.
Pamoja na hayo, sera za serikali za nchi za Ulaya dhidi ya wahamiaji na Uislamu, kwa muda mfupi, zinaweza kuwa kifuniko cha kuficha kufeli nchi hizo katika kuunda jamii yenye tamaduni nyingi katika kiwango cha maoni ya umma, lakini kwa muda mrefu, zitakuwa sababu ya kuongezeka migawanyiko ya kimbari, kidini, kikabila, kiuchumi na kijamii katika jamii za watu wa Ulaya na kuzidisha tishio kwa usalama na amani.