Waislamu nchini Slovakia hawana Msikiti, Serikali haiutambui Uislamu kuwa ni dini
https://parstoday.ir/sw/news/world-i120544-waislamu_nchini_slovakia_hawana_msikiti_serikali_haiutambui_uislamu_kuwa_ni_dini
Slovakia, iliyoko Ulaya ya Kati, ndiyo nchi pekee katika bara hilo ambayo haina hata msikiti mmoja licha ya kuwa na idadi kubwa ya Waislamu.
(last modified 2024-12-24T08:19:37+00:00 )
Dec 24, 2024 08:19 UTC
  • Waislamu nchini Slovakia hawana Msikiti, Serikali haiutambui Uislamu kuwa ni dini

Slovakia, iliyoko Ulaya ya Kati, ndiyo nchi pekee katika bara hilo ambayo haina hata msikiti mmoja licha ya kuwa na idadi kubwa ya Waislamu.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Shabestan, Waislamu wapatao elfu tano wanaishi nchini Slovakia, na ingawa nao pia ni sehemu ya jamii ya nchi hiyo ya watu wanaokaribia milioni 5.4 lakini wanachukuliwa kuwa ni raia wa daraja la pili na si dini yao wala mahitaji yao yanayopewa umuhimu wowote na serikali ya Bratislava.
 
Waislamu wa Slovakia wameomba mara kadhaa wawe na sehemu maalumu ya kufanyia ibada na hata wamewasilisha pendekezo kwa serikali la kujenga Msikiti, lakini kila mara wamekuwa wakipewa majibu ya kukataliwa.
 
Kwa mujibu wa Shabestan, sababu kuu inayopelekea Waislamu nchini Slovakia wakabiliwe na changamoto hiyo ni kwamba serikali ya nchi hiyo haitambui Uislamu kuwa ni dini na kiujumla ni kuwa jina la Uislamu limeondolewa kwenye orodha ya dini za nchi hiyo.
 
Ilikuwa ni mwaka 2016 ambapo serikali ya Slovakia ilitunga sheria ya kufuta jina la Uislamu katika orodha ya dini za nchi hiyo.
 
Taasisi ya Islamic Waqf Foundation, iliyoko katika mji mkuu Bratislava imeiomba mara kadhaa serikali ya Slovakia ikubali kujengwa Msikiti kwenye eneo la ardhi zilizotolewa na taasisi hiyo, lakini haijafanikiwa hadi sasa kupata ridhaa ya serikali.
 
Kutokubali kupokea wahajiri Waislamu ni moja ya sera kuu za serikali ya Slovakia, na moja ya visingizio inavyotumia kama sababu ya kutopokea wahajiri hao ni hiyo ya kutokuwepo hata Msikiti mmoja nchini humo.../