Trump analenga kunyakua ardhi za wengine ili kupanua ukubwa wa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/world-i120556-trump_analenga_kunyakua_ardhi_za_wengine_ili_kupanua_ukubwa_wa_marekani
Wakati bado Donald Trump hajaweka mguu wake kwa mara ya pili kwenye kiti cha urais wa Marekani, ameonesha mipango yake ya kupanua ardhi ya Marekani kwa kunyakua maeneo ya wengine.
(last modified 2024-12-24T09:56:18+00:00 )
Dec 24, 2024 09:56 UTC
  • Trump analenga kunyakua ardhi za wengine ili kupanua ukubwa wa Marekani

Wakati bado Donald Trump hajaweka mguu wake kwa mara ya pili kwenye kiti cha urais wa Marekani, ameonesha mipango yake ya kupanua ardhi ya Marekani kwa kunyakua maeneo ya wengine.

Baada ya juhudi za Trump za kudhoofisha mamlaka ya kitaifa ya Kanada, Mexico na Panama, sasa ni zamu ya Denmark ambapo inatakiwa kuiuzia Marekani kisiwa chake kikubwa na cha kistratijia cha Greenland. 

Kabla ya hapo, Trump aliwaambia kuwa kwa msingi wa kutokuwa salama kwa mipaka ya Kanada na Mexico dhidi ya uhalifu wa dawa za kulevya na kuingia kwa wahamiaji haramu nchini Marekani, alisema kuwa Kanada na Mexico zinapaswa kuwa majimbo ya hamsini na moja na hamsini na mbili ya Marekani.

Kuhusu Panama, Trump ameitisha kuwa ikiwa nchi hii haitapunguza ushuru kwa meli za Marekani zinazopita kupitia mfereji wa Panama, basi Marekani itachukua tena udhibiti wa njia hii muhimu ya baharini.

Hivi sasa, nchi nne, Kanada, Mexico, Panama, na Denmark zinakabiliwa na vitisho vya Marekani vya kunyakua ardhi zao punde   Donald Trump atakapoanza rasmi kazi yake katika Ikulu ya White House.

Jambo muhimu la kuzingatia ni kwamba nchi hizi nne zote ni washirika wa karibu wa Marekani, na kati yao, Kanada na Denmark ni wanachama wa muungano wa kijeshi unaojulikana kama Shirika la Mkataba wa Atlantiki Kaskazini – NATO ambalo linaongozwa na Marekani.

Vitisho vya Trump vya kunyakua ardhi za wengine ni kisingizio tu kwani inaonekana kwamba Marekani ya Trump ina malengo ya kisiasa ya ndani ya nchi na vita vya kibiashara vya kimataifa. 

Kwa mtazamo wa wale wenye misimamo mikali ya utaifa nchini Marekani, ambao sasa wamechukua madaraka wakiongozwa na Trump, Marekani haina budi ila kuhifadhi nafasi yake katika uga wa kimataifa isipokuwa iingie kwenye vita vya kiuchumi na madola ambayo yanaongoza kiuchumi duniani.

Nchi hizo zinajumuisha China na Russia, na makundi mawili ya kiuchumi duniani ambayo ni Umoja wa Ulaya na BRICS. Trump ameandaa mipango ya maalumu ya kukabiliana kiuchumi na madola hayo na pia madola mengine yote ambayo yanaonekana na washindani wa kiuchumi.

Kwa mfano, udhibiti wa Mfereji wa Panama ni muhimu kwa kukatiza uwezo wa China kufika kwa urahisi katika masoko ya bara Amerika, na Greenland ina nafasi ya kimkakati katika Bahari ya Atlantiki ya Kaskazini na katika mipaka ya bara Amerika, bara Ulaya na Aktiki.

Katika kukabiliana na muungano wa  BRICS ambapo Russia, China na Iran ni wanachama muhimu, Trump ameahidi kuwa iwapo nchi wanachama wa muungano huo zitatekeleza mpango wa kutupilia mbali sarafu ya dola ya Marekani, basi zitakabliwa na ushuru mzito wa Marekani.

Trump hajawahurumia hata waitifakia wa Marekani kwani ametishia kuwa iwapo Umoja wa Ulaya hautanuanua mafusa na gesi zaidi kutoka Marekani basi bidhaa za nchi hizo zitatozwa kiwango kikubwa cha ushuru kabla ya kuingia katika soko la Marekani.

Mambo haya yote yanaonyesha kwamba vitisho vya kunyakua ardhi za wengine ni utangulizi wa vita vya kiuchumi duniani ambavyo Trump anafanya juu chini kuhakikisha kuwa nchi yake inaibuka mshindi.

Trump anatarajia kutegemea nguvu za kijeshi za Marekani kuwashinikiza washirika wake wa kisiasa - kibiashara  kukabidhi mamlaka yao ya kitaifa na eneo kwa Marekani au, ikiwa lengo hilo halitatimia ataanzisha vita vya kibiashara vya kimataifa ili kuhakikisha nara yake ya "Marekani Kwanza" inatimia.