Ulyanov: Nchi za Magharibi zinazuia mazungumzo kati ya Iran na IAEA
-
Mikhail Ulyanov
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika mashirika ya kimataifa yenye makao yake makuu mjini Vienna amesema mbinu haribifu za nchi za Magharibi ni kikwazo cha maendeleo katika mazungumzo kati ya Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ili kusuluhisha masuala ambayo bado hayajatatuliwa.
Kuhusu mwenendo wa mazungumzo kati ya Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, Mikhail Ulyanov amesema: Safari ya Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa wakala huo nchini Iran katikati ya mwezi Novemba na kukutana kwake na maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu, kumeandaa mazingira mazuri ya kuwasiliana na serikali mpya ya Iran kupelekeka kufikiwa makubaliano muhimu.
Ulyanov ameongeza kuwa, "Ni makosa kusema kwamba hakuna maendeleo yaliyopatikana katika mazungumzo kati ya Iran na IAEA, ingawa harakati hii ina mipaka na mara kwa mara inakabiliwa na vikwazo maalumu. Amesema: Nchi za Magharibi, hasa Marekani, Uingereza, Ujerumani, na Ufaransa, zinatumia mbinu ya uharibifu, badala ya kuunga mkono maelewano hayo na kuweka mazingira yanayofaa kwa ajili ya utekelezaji wake.
Mwakilishi wa Kudumu wa Russia katika mashirika ya kimataifa mjini Vienna amesema: "Walipendekeza azimio dhidi ya Iran katika kikao cha Novemba cha Bodi ya Magavana wa IAEA, ambalo liliidhinishwa na nchi nyingi za Magharibi." Katika kujibu azimio lisilo la kujenzi la Baraza la Magavana, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitangaza kuzindua mashinepewa mpya na za kisasa katika vituo vyake vya kuzalisha nishati nyuklia.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikisisitiza kwamba itaendeleza ushirikiano wake na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ndani ya fremu ya makubaliano ya JCPOA na kwamba masuala yaliyosalia ya ulinzi yanaweza kutatuliwa kwa njia ya kitaalamu na bila ya upendeleo wa wakala huo.