Maandamano makubwa yafanyika Paris kuunga mkono Palestina
(last modified Sun, 12 Jan 2025 12:34:42 GMT )
Jan 12, 2025 12:34 UTC

Mji mkuu wa Ufaransa Paris umeshuhudia maandamano makubwa ya kuunga mkono Palestina na kulaani jinai za utawala dhalimu wa Israel katika Ukanda wa Gaza.

Wafuasi wa wananchi wa Palestina nchini Ufaransa wamefanya maandamano makubwa kulaani jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza na kutoa mwito wa kukomeshwa mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina.

Waandamanaji hao wakiwa wamebeba mabango na maberamu walipiga nara kama vile "Israel ni muuaji", "Palestine ibakie hai" na "Israel inaua watoto wa Kipalestina", wakitaka kukomeshwa kwa mauaji ya halaiki na ukoloni.

Mbali na Paris Ufaransa miji mingine mikubwa barani Ulaya imeshuhudia maandamano makubwa ya kulaani jinai za Israel na kutangaza himaya na uungaji mkono kwa wananchi wa Palestina.

Wito wa waandamanaji hao ni kusitishwa vita na kufunguliwa njia ya kufikishwa misaada ya kibinadamu kwa wananchi wa Ukanda wa Gaza wanaokabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu.

Kingine kinachopigiwa kelele na kulaaniwa na waandamanaji wanaoiunga mkono Palestina katika mataifa mbalimbali ulimwenguni ni mashambulio ya Israel dhidi ya hospitali na vituo vya matibabu.

Waandamanaji hao wametoa wito wa kuachiliwa huru daktari Hussam Abu Safiya, Mkugenzi Mkuu wa Hospitali ya Kamal Adwan ambaye alitiwa mbaroni hivi karibuni na wanajeshi wa Israel na kupelekwa kusikojulikana.