Marekani yaendelea kuteketea kwa moto
Hadi hivi sasa serikali ya Marekani imeshindwa kuzima moto mkubwa uliolikumbwa jimbo la California huku taarifa zikisema kuwa, takriban nyumba na maeneo ya biashara 35,000 ya mji wa Los Angeles yamekatikiwa na umeme na serikali ya Marekani imeshindwa kuwarejeshea wananchi huduma hiyo muhimu sana.
Shirika la Utangazaji la IRIB limetangaza kuwa, idadi ya vifo katika mji wa Los Angeles inaendelea kuongezeka. Vifo vilivyothibitishwa ni vya watu 16 lakini ni mapema mno kujua idadi hasa kwani kuna idadi kubwa ya watu hawajulikani walipo.
Kufikia sasa, ekari 40,000 za ardhi zimeshateketea kwa moto katika kaunti tano za Palisades, Eaton, Kenneth, Hurst na Lydia huko magharibi na kaskazini mwa Los Angeles nchini Marekani. Majengo 12,000 yakiwemo majengo mengi ya kifakhari ya mamilionea na watu mashuhuri, yameteketea kwa moto.
Rais kizee wa Marekani, Joe Biden ametangaza hali ya hatari huko California. Maafisa wanahofia moto huo unaweza kuenea mbali zaidi ya ulipofika hivi sasa, huku hali ya hewa ikitabiriwa kuzidi kuwa mbaya katika muda wa saa 72 yaani siku tatu zijazo.
Takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa wateja wapatao 20,000 wa kaunti ya Edison huko California bado hawana nishati katika kipindi hiki cha baridi kali. Pia, wateja wapatao 16,000 wa Idara ya Maji na Nishati ya Los Angeles (LADWP) nao hawana umeme.
Televisheni ya Sky News imeripoti kutokea jambo lisilo la kawaida linaloitwa kimbunga cha moto. Hali hiyo hutokea kwa sababu ya joto kali linalosababishwa na moto ulioenea sana, kama vile moto wa misitu na nyika na inakuwa vigumu kuuzima.