Ynetnews: Trump amemuahidi Netanyanu atamruhusu akiuke makubaliano mapya ya Ghaza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i121462-ynetnews_trump_amemuahidi_netanyanu_atamruhusu_akiuke_makubaliano_mapya_ya_ghaza
Rais mteule wa Marekani Donald Trump ameahidi kumruhusu waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu aanze tena kufanya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Ghaza baada ya kutia saini makubaliano yanayotarajiwa kutangazwa wakati wowote kutoka sasa ya kusitisha mapigano na harakati ya Hamas. Hayo yameelezwa na duru za habari za Israel.
(last modified 2025-01-15T08:01:44+00:00 )
Jan 15, 2025 08:01 UTC
  • Ynetnews: Trump amemuahidi Netanyanu atamruhusu akiuke makubaliano mapya ya Ghaza

Rais mteule wa Marekani Donald Trump ameahidi kumruhusu waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu aanze tena kufanya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Ghaza baada ya kutia saini makubaliano yanayotarajiwa kutangazwa wakati wowote kutoka sasa ya kusitisha mapigano na harakati ya Hamas. Hayo yameelezwa na duru za habari za Israel.

Ynetnews, imenukuu chanzo chenye taarifa suala hilo, kikiripoti jana Jumanne kuwa Trump amemuahidi Netanyahu kwamba ikiwa atakubali kusitisha mapigano na kuondolewa vikosi vya jeshi la Israeli kutoka Ghaza, ataiunga mkono Tel Aviv papo hapo ikiwa itaamua kuanzisha tena vita na kukiuka makubaliano hayo.
 
Katika andiko aliloweka kwenye mtandao wa X, mwandishi wa habari wa Palestina Muhammad Shehada amebainisha pia zaidi ya hayo akisema, Trump alikuwa amemuahidi Netanyahu kuondoa vikwazo kwa kampuni yenye utata ya NSO Group, ambayo imeziuzia nchi kadhaa virusi vya 'spyware' vya Pegasus, ambavyo ni moja ya vifaa maarufu zaidi vya udukuzi duniani.
 
" 'Zawadi' ya Trump inauruhusu pia utawala wa Israel kuendelea na unyakuzi wake wa ardhi katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu", ameongezea kueleza Shehada katika andiko lake hilo.
 
Netanyahu amekataa msururu wa mapendekezo ya kusitisha mapigano aliyowekewa mbele yake, likiwemo pendekezo lililotolewa na serikali ya Biden mwezi Mei 2024.

Hata hivyo mashinikizo ya umma na ya kidiplomasia dhidi ya utawala wake yamekuwa yakiongezeka kuutaka ufikie makubaliano ya kusitisha vita ili kuachiwa huru mateka wa Kizayuni wanaoshikiliwa Ghaza na mahabusu wa Kipalestina wanaoteseka kwenye magereza ya utawala huo wa Kizayuni.

Kwa upande wao, makundi ya Muqawama wa Wapalestina yameonyesha muda wote kuwa na nia ya kufikia makubaliano ya kusimamisha vita ili kuhitimisha mateso makubwa wanayohimili Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza.../