Kuchukizwa na Uzayuni, Safari Hii Uhispania
Timu ya Maccabi Tel Aviv imeibua tena hisia kali barani Ulaya, ambapo mechi ya timu ya mpira wa kikapu ya klabu hiyo huko Uhispania iliwakutanisha maelfu ya waandamanaji mitaani.
Maelfu ya watu jijini Madrid waliandamana wakiwa na mabango yanayosema kuwa Israel inatumia michezo kuficha uhalifu wake katika Ukanda wa Gaza.
Maandamano haya ya kuunga mkono Palestina yaliandaliwa na mashirika kadhaa ya kiraia yanayounga mkono Palestina na chama cha mrengo wa kushoto cha Uhispania, Podemos.
Waandamanaji walipeperusha bendera za Palestina huku wakipaza sauti za kauli mbiu kama vile, "Piga marufuku utawala wa Kizayuni," "Israel ni mwuaji," "Komboa Palestina," na "Mbele kwa mapambano ya ukombozi wa Palestina."
Katibu Mkuu wa Podemos, Ione Belarra, alikosoa kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania, Jose Manuel Albares, aliyesema kuwa "michezo inapaswa kutenganishwa na siasa.*
Kauli ya Albares ilikuja baada ya wito wa kuzuia kuingia kwa timu ya Maccabi Tel Aviv na mashabiki wake jijini Madrid.
Katibu Mkuu wa Podemos alisema: "Wakati Albares alianzisha juhudi katika Umoja wa Ulaya kuiondoa Russia kutoka shughuli za michezo kutokana na uvamizi wake nchini Ukraine, sasa anatetea utenganishaji wa michezo na siasa kuhusu Israel, ambayo inafanya mauaji ya kimbari. Huu ni unafiki na kushirikiana katika uhalifu na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina yanayofanywa na Israel."
Mwezi mmoja uliopita, wachezaji wa timu ya mpira wa miguu ya Maccabi walikumbana na maandamano makali dhidi ya uzayuni huko Uholanzi na Ufaransa. Waandamanaji waliokuwa na hasira walitangaza kupinga ukatili wa wafuasi wa Kizayuni wanaounga mkono Maccabi Tel Aviv. Maandamano hayo yalienea haraka jijini Amsterdam.
Hata kama Maccabi Tel Aviv inashika nafasi ya mwisho kwenye ligi ya Ulaya na mara nyingi hupoteza mechi zake, uwepo wa timu hiyo barani Ulaya safari hii umeibua hisia kali zaidi kuliko miaka ya nyuma.
Uhamasishaji huu ni matokeo ya mwamko katika fikra za umma katika nchi za Magharibi kuhusu utambulisho wa kibaguzi wa utawala wa Israel baada ya zaidi ya miezi 15 ya mauaji ya kimbari ya Wapalestina huko Gaza.
Katika michezo ya timu za utawala wa Kizayuni barani Ulaya, jambo linaloonekana wazi ni kushindwa kwa propaganda za kuutaja upinzani dhidi ya Israel kama eti ni chuki dhidi ya Wayahudi.
Kabla ya Oktoba 2023, miji ya Ulaya haijawahi kushuhudia maandamano makubwa na ya mfululizo dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel, lakini tangu Oktoba 7, 2023, kila mpenda haki, bila kujali msimamo wa kisiasa au wa kidini, anaonyesha wazi upinzani wake dhidi ya Isarel na Uzayuni bila hofu ya kushutumiwa kwa chuki dhidi ya Wayahudi.
Wazayuni na wanasiasa wengi wa Ulaya wamejaribu kufunika mauaji ya kimbari ya Wapalestina kwa kudai kuwa upinzani wowote dhidi ya Israel ni chuki dhidi ya Wayahudi. Mbinu hii sasa imepoteza itibari barani Ulaya na watu wanatamka wazi kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel ni utawala wa kikatili unaotenda jinai.
Wahalifu wa Kizayuni sasa wako kwenye hali ya wasiwasi duniani kote. Hivi sasa sio tu Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Waziri wa Vita wa zamani Yoav Gallant wanaosakwa kimataifa baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kutoa kikbali cha kuwakamata. Vyombo vya habari vya Kizayuni vimeiripoti kuwa wanajeshi wawili wa Israel walikamatwa hivi karibuni nchini Mexico. Wiki iliyopita, pia, jaji mmoja wa Brazil alitoa amri ya kukamatwa kwa mwanajeshi wa Kizayuni kwa madai ya uhalifu wa kivita, na mwanajeshi huyo alilazimika kutoroka usiku kutoka nchini humo.
Gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth liliripoti kuwa malalamiko yamewasilishwa dhidi ya Ghassan Alian, jenerali maarufu wa jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel wa kikosi cha COGAT, ambaye anaishi kwa siri nchini Italia. Kuna uwezekano wa yeye kukamatwa kwa uchunguzi wa uhalifu wa kivita.
Kutokana na hali hii, Wizara ya Mambo ya Nje ya utawala wa Kizayuni imewashauri Wazayuni wanaoishi katika ardhi za Palestina zilizokaliwa (Israel) hususan wanaohudumu katika jeshi la utawala huo, kuepuka safari zisizo za lazima katika nchi zilizotia saini Mkataba wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu.