Maelfu waandamana London Uingereza kuunga mkono Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/world-i121612-maelfu_waandamana_london_uingereza_kuunga_mkono_palestina
Maelfu ya wafuasi wa Palestina wameandamana katika mji mkuu wa Uingereza London na kutoa wito wa kutekelezwa kikamilifu makubaliano ya kusitisha vita kati ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2025-01-18T23:08:59+00:00 )
Jan 18, 2025 23:08 UTC
  • Maelfu waandamana London Uingereza kuunga mkono Palestina

Maelfu ya wafuasi wa Palestina wameandamana katika mji mkuu wa Uingereza London na kutoa wito wa kutekelezwa kikamilifu makubaliano ya kusitisha vita kati ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Waandamanaji hao walikusanyika mbele ya ofisi ya Waziri Mkuu  wa nchi hiyo Keir Starmer na kutaka kutekelezwa kikamilifu usitishaji vita huko Gaza, kukomesha ukaliaji mabavu  wa utawala wa Kizayuni dhidi ya ardhi ya Palestina na kusitishwa uungaji mkono wa kijeshi na kisiasa wa London kwa Tel Aviv.

Waandamanaji hao wakiwa wamebeba mabango na maberamu pamoja na bendera za Palestina walisikika wakipiga nara kama "Iacheni Palestina iwe huru" na "Acheni kuiunga mkono Israel".

Waandamani hao wamelaani vikali hatua ya serikali ya Uingereza ya kuiunga mkono serikali ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu na kutaka kukomeshwa uungaji mkono huo.

Tangu kuanza hujuma na mashambulio ya kinyama ya utawala dhalimu wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza, miji mbalimbali ya Uingereza hususan mji mkuu London kila mara imekuwa ikishuhudiwa maandamano makubwa ya kuunga mkono Palestina na kulaani jina za Israel na uungaji mkono wa nchi hiyo ya bara Ulaya kwa utawala huo ghasibu.