Nebenzya: Marekani ndiyo sababu ya mgogoro katika Asia Magharibi
-
Vasily Nebenzya
Mwakilishi wa kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa: Kushadidi mgogoro wa sasa katika eneo la Asia Magharibi, ambao haujawahi kuonekana hapo kabla, ni matokeo ya sera mbaya za Marekani.
Vasily Nebenzya amesema: "Machafuko katika eneo la Asia Magharibi yanatokana na operesheni za kijeshi zisizo na kifani za utawala wa Israel ambazo zimepata uungaji mkono na msaada usio na mpaka wa kijeshi na kimataifa kutoka Washington."
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Russia katika Umoja wa Mataifa amesema: "Sera mbaya za Marekani hazijafanya lolote ila kuibua hali ya mgogoro ambayo sasa inahusisha eneo zima la Asia Magharibi, raia na walinda amani."
Wakati huo huo, Seneta wa Marekani, Bernie Sanders amesema katika taarifa yake kwamba Washington imeshiriki katika kutekeleza mauaji ya kimbari na jinai huko Gaza kwa kutuma silaha kwa Benjamin Netanyahu.
Karibu Wapalestina elfu 50 wameuawa na maelfu ya wengine hawajulikani waliko kufuatia mauaji ya kimbari ya utawala huo dhidi ya raia wa Palestina yaliyoendelea kwa kipindi cha miezi 15.