Christopher Hedges: Nasikitishwa na tabia ya kuwataja Waislamu kuwa ni mashetani
-
Chris Hedges
Mwandishi wa habari wa Marekani, Christopher Hedges, amesema anasikitishwa na jinsi Waislamu wanavyodhihirishwa katika nchi za Magharibi katika sura ya mashetani akisisitiza kwamba utamaduni wa Kiislamu ni tofauti kabisa na sura potovu inayowasilishwa.
Chris Hedges ameyasema hayo katika kipindi cha “The Interview,” cha televisheni ya al Jazeera ya Qatar akizungumzia tajriba yake ya uandishi wa habari katika vyombo vya habari vya Marekani, na kuhusu msimamo wake juu ya sera za nchi yake, hasa upinzani wake dhidi ya uvamizi wa Iraq na Afghanistan na uungaji mkono usio na mpaka wa Marekani kwa Israel.
Hedges, ambaye pia ni mwandishi na mchambuzi, ameishi kwa miaka saba Mashariki ya Kati, na anasema kwamba alifahamiana na Waarabu na kujifunza lugha na utamaduni wao, na kwa kuzingatia hilo, anapinga unyanyasaji wa nchi za Magharibi wa kuwatambulisha Waislamu kuwa ni mashetani.
Mwandishi huyo wa habari wa Marekani ameeleza upinzani wake dhidi ya uvamizi wa nchi yake huko Iraq na Afghanistan na kusema: "Uvamizi huo ulikuwa maafa makubwa sana kwa Wairaqi, Waafghani na pia kwa Marekani na kwamba ulikuwa ishara au dalili ya kuanguka kwa ufalme wa Magharibi."
Katika muktadha huohuo, Hedges anafafanua kuwa: “Ufalme wa Marekani ni taasisi ya uhalifu ambayo imesababisha mateso na vifo vya mamilioni ya watu ulimwenguni kote."
Amesema: "Israel isingeweza kutekeleza mauaji yake ya kila siku kama hatungeipatia silaha. Hili lazima likome," na kusisitiza kwamba "dola la Marekani linaiangamiza Marekani yenyewe, na halijui kufanya lolote sipokuwa kutengeneza silaha na kuanzisha vita."
Kuhusu sera zitakazofuatwa na Rais mteule wa Marekani, Donald Trump mkabala wa Israel, mwandishi huyo wa habari wa Marekani ameeleza kuwa, Trump atafanya chochote Israel inachotaka, na kwamba muhimu kwake yeye ni pesa na kumtii yeye.