Guterres: Misaada ya matibabu lazima iingie Gaza bila kizuizi chochote
https://parstoday.ir/sw/news/world-i121706-guterres_misaada_ya_matibabu_lazima_iingie_gaza_bila_kizuizi_chochote
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametangaza kuwa ili kuokoa maisha ya wagonjwa na kuwatibu waliojeruhiwa, msaada wa matibabu lazima uingie Gaza bila vikwazo vyovyote.
(last modified 2025-01-21T03:46:29+00:00 )
Jan 21, 2025 03:46 UTC
  • Antonio Guterres
    Antonio Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametangaza kuwa ili kuokoa maisha ya wagonjwa na kuwatibu waliojeruhiwa, msaada wa matibabu lazima uingie Gaza bila vikwazo vyovyote.

Antonio Guterres amezitaka pande zinazozozana katika Ukanda wa Gaza kushirikiana na Umoja wa Mataifa ili kuzuia uporaji wa misaada ya kibinadamu katika eneo hilo. Guterres ameeleza haya katika hotuba aliyoitoa kuhusu kuwanusuru wagonjwa na kuwapatia matibabu majeruhi huko Gaza. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia amezitolea wito pande mbili zinazozozana kufanya juhudi za kutekeleza usitishaji vita wa kudumu na kurejesha amani endelevu katika Ukanda wa Gaza. 

Guterres amesema kuwa juzi malori zaidi ya 630 yaliyobeba misaada ya kibinadamu yaliwasili Gaza na kwamba risasi ambazo hazijaripuka katika eneo hilo zinapasa kuondolewa. 

Katibu Mkuu wa UN ameongeza kuwa: Jitihada yoyote ya Israel ya kutaka kuyaunganisha maeneo ya Ukingo wa Magharibi na maeneo ya utawala huo ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.