Mayahudi wa Marekani: Israel imeshindwa katika vita vya Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i122118-mayahudi_wa_marekani_israel_imeshindwa_katika_vita_vya_gaza
Zaidi ya asilimia 80 ya jamii ya Wayahudi wa Marekani walioshiriki katika uchunguzi wa maoni wametangaza kuwa, Israel katu haijapata ushindi katika vita vya Gaza.
(last modified 2025-01-30T23:22:32+00:00 )
Jan 30, 2025 23:22 UTC
  • Mayahudi wa Marekani: Israel imeshindwa katika vita vya Gaza

Zaidi ya asilimia 80 ya jamii ya Wayahudi wa Marekani walioshiriki katika uchunguzi wa maoni wametangaza kuwa, Israel katu haijapata ushindi katika vita vya Gaza.

Tovuti ya habari ya Kiebrania ya "News One" imetangaza katika ripoti yake kwamba matokeo ya uchunguzi huo wa maoni yanaonyesha kuwa, zaidi ya asilimia 80 ya jamii ya Wayahudi wa Marekani wanaamini kuwa hakuna ishara yoyote ya ushindi wa Israel katika vita vya hivi karibuni vya Gaza.

Kulingana na matokeo ya uchunguzi huo, 33% ya Wayahudi wa Marekani walisema kuwa, makubaliano ya sasa ni ushindi kwa Hamas na kushindwa kwa Israel.

Asilimia 31 walisema kuwa, huo ni ushindi wa pamoja kwa pande zote mbili zilizohusika katika vita hivyo.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Umoja wa Mayahudi wa Ufaransa kwa ajili ya Amani (The French Jewish Union for Peace) UJFP umewahi kuishutumu Israel kwa "kuua Uyahudi" kutokana na mashambulizi yake ya kikatili unayofanya katika Ukanda Gaza na kueleza kwamba vyombo vya habari vya Israel vinapata burudani kwa mateso wanayopata Wapalestina.

Jumuiya hiyo imelaani vikali serikali ya utawala wa Kizayuni wa Israel kwa mashambulizi yake dhidi ya Gaza, ambayo imesema yameathiri pia jamii ya Israel, kwa sababu maoni ya umma ya sehemu kubwa ya jamii ya Waisrael yamejiweka mbali na ubinadamu.

Umoja wa Mayahudi wa Ufaransa kwa ajili ya Amani umewahutubu Wayahudi duniani kote ukisisitiza juu ya kuwepo sheria za kimataifa na haki za binadamu na kuwahimiza kuchukua msimamo wa pamoja wa kujipambanua na Israel ili kutoshirikishwa katika mauaji ya Israel.