Mbunge wa Ukraine aitaka EU imuue kigaidi Rais Putin
Mbunge wa Ukraine, Aleksey Goncharenko amewataka wazi wazi wabunge wa Umoja wa Ulaya kuunga mkono wazo la kuuawa Rais wa Russia, Vladimir Putin na kulipigia debe miongoni mwa watu wa kawaida.
Jana Ijumaa, mbunge huyo alisambaza video kwenye ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa Telegram, akitoa kauli zenye utata katika Kamati ya Bunge la Baraza la Ulaya (PACE).
Kwa mujibu wa Goncharenko, Kiev inaweza kuimarisha uungwaji mkono katika nchi za Magharibi kwa kutoa wito wa aina hiyo, eti unaoendana na matakwa ya msingi na yanayoeleweka kwa urahisi ya watu.
Mwanasiasa huyo amesema, "Ili kufanya hivyo, Ukraine inahitaji kuweka uwiano wa wazi kati ya kifo cha kiongozi wa Russia na manufaa ambayo kila raia wa EU anaweza kupata kutoka na kuuawa kwake."
"Tunahitaji kuwaonyesha watu kwa nini tunahitaji kufanya hivi," mwanachama huyo wa kikundi cha Mshikamano wa Ulaya katika Bunge la Kiev amesikika akiiambia Kamati ya Bunge la Baraza la Ulaya kwa lugha ya Kiingereza.
Ameongeza kwa kusema, "Hiki kisasi si chetu tu, huu ndio uwekezaji bora zaidi tunaoweza kufanya." Tunatafuta uwekezaji mkubwa. Uwekezaji bora zaidi duniani leo hii ni kumuua Putin,” amesisitiza mtunga sheria huyo wa Ukraine.