Nchi 9 zaunda 'Kundi la Hague' kutetea haki za Wapalestina
https://parstoday.ir/sw/news/world-i122172-nchi_9_zaunda_'kundi_la_hague'_kutetea_haki_za_wapalestina
Nchi tisa zimetangaza kuunda "Kundi la Hague" la kupigania haki za wananchi madhulumu wa Palestina.
(last modified 2025-02-01T03:52:16+00:00 )
Feb 01, 2025 03:52 UTC
  • Nchi 9 zaunda 'Kundi la Hague' kutetea haki za Wapalestina

Nchi tisa zimetangaza kuunda "Kundi la Hague" la kupigania haki za wananchi madhulumu wa Palestina.

Wawakilishi kutoka Afrika Kusini, Malaysia, Namibia, Colombia, Bolivia, Chile, Senegal, Honduras na Belize walikutana mjini The Hague nchini Uholanzi jana Ijumaa, katika mkutano ulioandaliwa na shirika la kimataifa la kisiasa la Progressive International, kuratibu hatua za kisheria, kidiplomasia na kiuchumi dhidi ya ukiukaji wa sheria za kimataifa wa Israel.

Kufuatia majadiliano yaliyofanyika katika mkutano huo, nchi hizo tisa zimetangaza kuunda Kundi la The Hague ambalo zinasema ni 'zao la dharura.'

Kundi hilo limesema linasikitishwa na wimbi la kupotea maisha, riziki, jamii na urithi wa kitamaduni kutokana na vitendo vya mauaji ya halaiki ya Israel katika Ukanda wa Gaza, na maeneo mengine ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu. Kundi hilo la 'Hague Group' limebainisha kuwa, haliwezi kuendelea 'kukaa kimya" mbele ya uhalifu kama huo wa kimataifa.

Kundi hilo limesema, "Tumedhamiria kushikamana na majukumu yetu ya kukomesha uvamizi wa Israel katika taifa la Palestina, na kuunga mkono kufikiwa kwa haki isiyoweza kufutika ya watu wa Palestina ya kujitawala, ikiwa ni pamoja na haki ya kuwa na taifa lao huru la Palestina."

Ikumbukwe kuwa, Mei mwaka jana, wataalamu na mawakili wa kujitegemea mjini The Hague walitangaza kuunga mkono uamuzi wa Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ya kuomba hati ya kukamatwa maafisa wa utawala ghasibu wa Israel, kwa kuhusika na jinai za kivita Gaza.