Mwanasheria Mmarekani: Israel imeua Wapalestina 360,000 Gaza
Mwanasheria mashuhuri wa Marekani na mwanaharakati wa haki za watu asilia anakadiria kuwa jeshi la Israel limewaua takriban watu 360,000 katika vita vyake vya mauaji ya kimbari vilivyodumu kwa muda wa miezi 15 katika Ukanda wa Gaza, akisema kwamba idadi ya vifo vya kweli katika eneo lililozingirwa ni kubwa zaidi kuliko takwimu iliyoripotiwa na vyombo vya habari.
Steven Donziger, ambaye alitumia miongo kadhaa akipambana na shirika la Chevron kuhusu uchafuzi wa mazingira katika msitu wa Ecuador, alisema hayo jana Jumatano, huku akikosoa idadi "finyu na isiyo kamili" ya vifo huko Gaza, ambayo inaripotiwa katika vyombo vya habari vya kimataifa.
Amesema, "Takwimu rasmi kutoka kwa Wizara ya Afya ya Gaza inaripoti takriban vifo 46,000, lakini takwimu hii inajumuisha tu vifo vya moja kwa moja kutokana na mashambulizi ya mabomu na makombora."
Mtaalamu huyo wa masuala ya sheria wa Marekani amesisitiza kuwa, idadi ya vifo inayoripotiwa haizingatii vifo visivyo vya moja kwa moja kutokana na njaa, magonjwa, na ukosefu wa huduma za matibabu unaosababishwa na uharibifu wa miundombinu ya afya ya Gaza, na mzingiro uliowekwa na Israeli.

Donziger amebainisha kwamba, kufikia Januari 19 mwaka jana 2024, idadi ya vifo huko Gaza, ikiwa ni pamoja na vilivyotokana na sababu za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, inaweza kuwa juu ya 360,000, kulingana na uchambuzi wake.
Takwimu za mwanasheria huyo aliyesomea katika Chuo cha Harvard zinatokana na utafiti uliochapishwa na jarida la matibabu la Lancet la Uingereza mnamo Juni 2023, kukadiria kuwa athari za vita vya Israeli dhidi ya Gaza zinaweza kupelekea idadi ya vifo kupindukia watu 186,000.