EU yamkingia kifua Zelensky baada ya kushambuliwa vikali na Trump
Mvutano kati ya Ulaya na Marekani umeendelea kushtadi, baada ya viongozi wa nchi kadhaa za Umoja wa Ulaya kumkingia kifua Rais Vladimir Zelensky wa Ukraine, aliyeshambulia kwa maneno makali na Rais Donald Trump wa Marekani hivi karibuni.
Viongozi hao wa Ulaya, wakiwemo wale wa Uingereza, Ujerumani, na Jamhuri ya Czech, wametangaza kumuunga mkono Zelensky baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kumtaja kama "dikteta asiyechaguliwa."
Katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social siku ya Jumatano, Trump alimshutumu kiongozi huyo wa Ukraine kwa kusimamia vibaya mzozo na Russia na kutumia vibaya misaada ya kifedha ya Marekani.
Trump amedai kwamba Zelensky "anakataa kuwe na uchaguzi" na kwamba "yuko chini sana katika tafiti za maoni Ukraine." Wadadisi wa mambo wanaamini kuwa, ujumbe huo mzito wa Trump yumkini ulichochewa na shutuma kutoka kwa Zelensky kwamba Rais huyo wa Marekani amezama kwenye bahari ya habari za upotoshaji za Russia.
Haya yanajiri siku chache baada ya Wabunge wa Bunge la Ulaya kusema kuwa, bara hilo haliwezi kuendelea kuitegemea kikamilifu Marekani katika masuala ya ulinzi; na kutoa wito wa kuimarisha uwezo wa kiulinzi wa Ulaya sambamba na kuendelea kuiunga mkono Ukraine.
Weledi wa mambo wanasema kuwa, Umoja wa Ulaya unafuatilia kwa dhati kukomesha utegemezi wa ulinzi, wakati huu ambapo kunashuhudiwa mabadiliko ya vipaumbele vya sera za kigeni ya serikali mpya ya Marekani.